POLISI ANASWA AKICHANA MABANGO YA KAMPENI YA MGOMBEA

Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Hillary Mutyambai amethibitisha kuwa polisi wamechukua hatua dhidi ya afisa mmoja aliyenaswa kwenye kamera akiharibu mabango ya kampeni kutoka kwa gari la kampeni.

Katika taarifa siku yaJumapili, Machi 13, Mutyambai alibainisha kuwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho baada ya mwanasiasa ambaye mabango yake ya kampeni yaliharibiwa kuripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Kericho.


Polisi huyo alionyeshwa kwenye video aking’oa mabango ya kampeni kwenye gari la mwanasiasa Quenas Chepkemoi ambaye anawania kiti cha useneta katika kaunti ya Kericho.


“Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) imepokea malalamishi ya Chepkemoi ambaye mabango yake yaliyokuwa yamebandikwa kwenye gari lake yaliraruliwa na afisa mmoja wa polisi anayejulikana. DCI inayochunguza tukio hilo kwa hatua zinazofaa”, ilisoma taarifa hiyo kwa sehemu.


Mutyambai alielezea kusikitishwa na kisa hicho kinachomlenga mwaniaji huyo, na kuongeza kuwa uchunguzi wa kisa hicho utaharakishwa. “NPS inajutia tukio hilo, hasa ikilenga mwanamke anayewania nafasi hiyo. Tunataka kurudia hakikisho letu la juu zaidi kwa usalama wa wawaniaji wote na haswa wagombeaji wa kike.”

“Hakuna vitendo vya uhuni na kutovumiliana vinavyoelekezwa kwa makundi yaliyo hatarini, ikiwa ni pamoja na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vitavumiliwa kutoka sehemu yoyote, ikiwa ni pamoja na wale walio katika sheria,” IG alisema.

Huku akirejelea agizo lililotolewa na Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiangi, kuhusu usalama wa wagombea wa kike, Mutyambai aliwataka maafisa wa polisi kuwa waangalifu katika kuhakikisha usalama unakuwepo wakati huu wa uchaguzi.

Aidha, alibainisha kuwa idara yake imeweka utaratibu wa kukabiliana na aina zote za unyanyasaji ikiwa ni pamoja na dhuluma ya kijinsia, na wanyonge wengine wanaowania nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments