Dkt. TAX AELEZA MAFANIKIO YA MWAKA MMOJA YA WIZAYA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA

 Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax akiwa kwenye kikao na Waandishi wa habari katika ofisi za Wizara Mtumba Jijini Dodoma ambapo ameeleza mafanikio ya Mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita katika Wizara hiyo ikiwemo kuimarisha ulinzi wa mipaka ya Tanzania.

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog-DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa katika kipindi cha mwaka mmoja wa awamu ya sita imeingia kwenye mafanikio mengi ikiwemo kuhakikisha kuwa nchi ipo salama na amani inalindwa na kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nchi. 

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt. Stergomena Lawrence Tax katika kikao chake na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita tangu Rais Samia Suluhu Hassan aliposhika madaraka ya kuiongoza Tanzania. 

Amesema,Licha ya changamoto zilizojitokeza kwenye baadhi ya maeneo ,Wizara hiyo imeendelea kuwa kinara  kwenye utoaji mafunzo ya kijeshi katika Vyuo na shule za kijeshi ndani na nje ya nchi,utoaji mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa JKT na utoaji huduma za matibabu kwa wanajeshi na familia zao ,vijana wa JKT,watumishi wa Umma na wananchi.

"Tunaendeleea kustawi pia katika uhawilishaji wa Teknolojia kwa ajili ya kuzalisha mazao ya msingi,udumishaji wa ushirikiano kitaifa na kimataifa katika sekta ya ulinzi,utatuzi wa migogoro ya ardhi,ujenzi wa makao makuu ya ulinzi wa taifa na utoaji wa kipaumbele katika uendelezaji miradi ya kielelezo na kimkakati na ulipaji madeni ya wazabuni waliotoa huduma mbalimbali,"amesema.

Amefafanua kuwa kama lilivyo jukumu la Wizara hiyo katika kulinda taifa dhidi ya maadui toka ndani na nje ya nchi,itahakikisha nchi inakuwa salama na kulinda amani ikiwa ni pamoja na kuimarisha mshikamano baina yake na wananchi wake.

Amesema,Kwa kipindi cha mwaka mmoja, Serikali imeiwezesha Wizara hiyo kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa weledi,umakini na mafanikio hivyo kuwezesha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu ikiwa ni pamoja na kulipa madeni yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 175 kwa wazabuni waliotoa huduma mbalimbali.

"Hii imejenga imani kwa Serikali na kuiwezesha Wizara kuendesha majukumu yake ya msingi kwa ufanisi,na tutaendelea kusimama zaidi katika kulinda amani ambapo wizara hii kupitia JWTZ inaendelea kuondoa changamoto chache katika baadhi ya mipaka hususani Kusini na hivyo tupo salama,"amefafanua Waziri huyo.

Akifafanua kuhusu migogoro ya ardhi iliyotatuliwa na Wizara hiyo ambayo inahusisha maeneo ya jeshi na wananchi ,Dkt.Tax amesema migogoro ipatayo 74 tayari imeshughulikiwa huko Arusha.

Kadhalika Serikali pia imeendelea kudumisha ushirikiano wa kimataifa na kitaifa kupitia sekta ya ulinzi hususani kushirikiana na umoja wa mataifa (UN),Umoja wa Afrika(AU)na Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC)katika operesheni mbalimbali za Ulinzi wa amani kwa kupeleka vikosi na usaidizi,waangalizi wa Jeshi na makamanda katika nchi zenye migogoro.

"Chini ya Serikali ya awamu ya sita , JWTZ linavyo vikosi vya Ulinzi wa amani katika nchi za Lebanon,Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Kongo na Jamhuri ya kati,Jeshi hili pia linashiriki katika kamisheni ya SADC (SAMIM)katika kupambana na ugaidi huko Msumbiji,"ameeleza

Pamoja na hayo ameeleza kuwa ili kuwa na Taifa imara , Serikali imeendelea kutoa mafunzo ya awali ya kijeshi kwa vijana wa mujibu wa sheria na vijana wa kujitolea kwa lengo la kujenga uzalendo na ukakamavu ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi adhima ya kuwajengea vijana stadi na uwezo wa kujitegemea.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments