WAFANYABIASHARA WAASWA KUFICHUA WATU WANAOJIFANYA ASKARI POLISI KWA LENGO LA KUJIPATIA KIPATO


Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala ACP Debora Magiligimba amewaomba wafanyabiashara kutoka maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Kipolisi Ilala kutoa ushirikiano pindi wanapokumbana na kadhia kutoka kwa baadhi ya watu wanaojifanya ni askari polisi na kufanya kazi za kuhoji uhalali wa nyaraka mbalimbali za malipo ya biashara kwa nia ya kujipatia kipato huku wakilichafua jeshi la polisi.
 
Kamanda Magiligimba ameyasema hayo 11/03/2022 ofisini kwake  wakati akiongea na baadhi ya wafanya biashara wa soko la  Kariakoo ambao aliwaita kuja  kueleza changamoto wanazokutana nazo katika biashara zao.

 Aidha,  Kamanda Magiligimba aliwapatia  wafanyabiashara hao  namba za viongizi wa Polisi ili wanapoona kama kuna watu wa aina hii katika maeneo yao ya biashara waweze kutoa taarifa mapema iwezekanavyo.

"Niwaombe kutoa taarifa/ushirikiano wa haraka kwa Jeshi la Polisi pindi mnapoona kuna viashiria vyovyote vya uhalifu unaofanywa na watu wanaojifanya ni askari polisi ili tuweze kuushughulikia kabla uhalifu haujafanyika. Lengo letu ni kuhakikisha wafanyabiashara mnafanya biashara zenu kwa amani  na utulivu ili kuongeza pato la Taifa kwa kulipakodi",alisema Kamanda Magiligimba.

Naye mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka kutajwa jina lake amelipongeza jeshi la Polisi na kusema kuwa kwa sasa wanaona askari polisi wakifanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za jeshi la polisi tanzania na badala yake kumeibuka kikundi cha watu wanaojitambulisha ni askari polisi na kuanza kuwabughudhi katika biashara zao kwa kudai/kuhoji risiti kwa kila mzigo.

"Niwe mkweli tu kwamba siku hizi naona mabadiliko makubwa sana ndani ya Jeshi la Polisi kwani zamani kulikuwa na tabia kwa baadhi ya askari polisi kufanya matendo kinyume na maadili lakini sasa hivi vitendo hivyo hakuna na badala yake kuna baadhi ya watu wameibuka na kuanza kujitambulisha wao ni askari polisi na 8kuanza kuwababaisha kuwa wanataka  uhalali wa nyaraka lasivyo wanawapeleka kwenye mamlaka ya mapato na endapo utaomba msaada kwa jeshi la polisi basi watu hao hukimbia",alisema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post