UMOJA WA MATAIFA WAITAKA URUSI KUSIMAMISHA MARA MOJA MASHAMBULIZI NCHINI UKRAINEBaraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) limepiga kura kwa wingi ya kuunga mkono azimio la kuitaka Urusi kusimamisha mara moja mashambulizi nchini Ukraine na kuyaondoa majeshi yake yote nchini humo.

Mataifa mengi wanachama wa umoja huo yameonyesha kuliunga mkono azimio hilo. Kura hiyo iliyoitwa “uvamizi dhidi ya Ukraine” ilipigwa katika kikao cha dharura cha baraza hilo. Kwenye kura hiyo mataifa 141 yaliunga mkono azimio hilo, na kupingwa na mataifa matano, na 35 hayakuwepo kwenye mchakato wa kupiga kura.


Urusi iliungwa mkono na Belarus, Syria, Korea Kaskazini na Eritrea, dalili inayoashiria namna taifa hilo lilivyotengwa kimataifa kufuatia uvamizi huo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwaambia waandishi wa habari baada ya kura hiyo kwamba ujumbe wa UNGA uko wazi na ni dhahiri kwamba Urusi inatakiwa kusimamisha mashambulizi Ukraine mara moja na kufungua milango ya mazungumzo na diplomasia.

Balozi wa Cuba ambayo haikuwepo kupiga kura Pedro Luis Cuesta amelaumu kuhusu mzozo huo akisema umechochewa na matamanio ya Marekani ya kupanua jumuiya ya NATO eneo la mashariki na kuelekea kwenye mipaka ya Urusi pamoja na kupeleka silaha za kisasa nchini Ukraine huku ikipuuza wasiwasi wa Urusi juu ya usalama wake.

Kabla ya kura hiyo, balozi wa Ukraine kwenye umoja huo Sergiy Kyslytsya alisema vikosi vya Urusi vimeingia kwenye ardhi ya Ukraine sio tu kuwaua baadhi ya watu lakini pia kuchukua haki ya Ukraine ya kuendelea kuwepo na kuongeza kuwa uhalifu ni wa kutisha mno.

Maandishi yanayomaanisha “inusuru Ukraine” huko Bulgaria kama moja ya njia ya kupeleka ujumbe wa kupinga taifa hilo kuvamiwa.


Balozi wa Urusi, Vassily Nebenzia yeye aliuomba umoja huo kulikataa azimio hilo akidai mataifa ya magharibi yaliongeza shinikizo lisilo kifani sambamba na vitisho vya wazi ili kuungwa mkono. Azimio hilo pia limelaaini uhusika wa Belarus kwamba ilitumia nguvu dhidi ya Ukraine.

Na huko Jerusalem, kansela wa Ujerumani Olaf Cholz pamoja na waziri mkuu wa Israel Naftali Bennet jana walisisitizia wajibu wao katika kuhakikisha kunafanyika mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine.


Scholz alithibitisha wajibu wa Ujerumani kwa usalama wa Israel akisema tayari taifa lake lilishaweka wazi kuhusu hilo na kuongeza kuwa kwa pamoja na Israel walikuwa na nia ya dhati kushirikiana ili kuhakikisha mazungumzo zaidi ya amani kati ya Urusi na Ukraine, huku Bennet akisema wanawajibika pia kuzuia umwagikaji wa damu.

Nchini Ufaransa, rais Emmanuel Macron amesema Ulaya imeingia kwenye enzi mpya baada ya Urusi kuivamia Ukraine. Amesema katika hotuba yake kupitia televisheni kwamba kutokana na hali hiyo wanalazimika kufanya maamuzi na kurudia mwito kwa Ulaya kusimamia usalama wake badala ya kutegemea wengine. Macron aidha amelimwagia sifa jeshi la Ukraine lakini akionya kwamba siku zijazo huenda zikawa ngumu zaidi.


Mmiliki wa klabu ya Chelsea Roman Abramovich atangaza kuiuza klabu hiyo na kupeleka fedha kwa wahanga wa vita, Ukraine

Mjini The Hague, mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu ICC imetangaza kuanzisha uchunguzi rasmi wa wa uhalifu wa kivita unaofanyika dhidi ya watu wa Ukraine. Mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Karim Khan amesema tayari ameifahamisha ofisi ya rais wa ICC kuhusu hatua yake ya kuendeleza uchunguzi na tayari wameanza kukusanya vithibitisho. Ikumbukwe tu kwamba Urusi haijasaini Mkataba wa Rome ulioanzisha mahakama hiyo.


Huko Uingereza, mmiliki wa klabu ya klabu ya Premier ya Chelsea Roman Abramovich ameamua kuiweka mauzoni timu hiyo na kuahidi fedha zitakazopatikana atazitoa kwa wahanga wa vita nchini Ukraine.

Kulingana na ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, watu 227 wamekufa na 525 kujeruhiwa hadi usiku wa kuamkia jana nchini Ukraine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post