MTAKA APANIA KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI MZAKWE


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka akiongea na watendaji,wadau wa mazingira na wanakijiji walikuwa wakiishi jirani na eneo la hifadhi ya maji Mzakwe-Dodoma kuhusu namna ya kuendeleza upya zoezi la upandaji wa miti inayoendana na hali ya udongo wa eneo hilo.
Muonekano wa eneo la  Bonde la mto Wami/Ruvu-Mzakwe Jijini Dodoma ambalo Serikali inafanya jitihada za kunusu uhifadhi wake kwa kupanda miti

***

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 blog-DODOMA

WANANCHI waliohamishwa katika vijiji vya Ilindi, Mzakwe,Gawaye na Mundemu kwa ajili ya kupisha chanzo cha bonde la mto Wami-Mzakwe jijini Dodoma wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka kuingilia kati suala la kulipwa fidia zinazoendana na thamani ya maeneo yao ili kuondokana na migogoro ambayo inadhaniwa kuwa huenda inasababisha miti kushindwa kuota kwenye eneo hilo.

Hatua hii imekuja kufuatia Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma jana kufanya ziara katika eneo hilo kutafuta suluhu ya namna ya kuotesha miti katika eneo hilo ambalo limekuwa sugu licha Serikali kutumia nguvu kubwa za kustawisha miti ya aina mbalimbali jambo ambalo wenyeji hao wamedai inawezekana linatokana na manung'uniko yao.

Mzee Shaban Nyambo amesema mfumo uliotumika kuwaondoa katika maeneo yao haukuzingatia haki za binadamu na kwamba hata malipo ya fidia zao hayakuendana na thamani halisi ya maeneo yao jambo lililopelekea badhi yao kushindwa kumudu gharama za maisha na kuishia kuwa maskini.

"Ukimsababishia mtu manung'uniko huwezi kufanikiwa,eneo hili limekuwa sugu miti haioti, Serikali imeelekeza jitihada zote lakini bado, inawezekana kabisa hili linatokea kwa sababu bado mioyo yetu haina amani,hatujalipwa vizuri,kuna watu wamelipwa mpaka laki tatu wengine laki moja hi haifai,"amesema.

Kutokana na hayo,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony mtaka ameziagiza taasisi zote zinazohusika na uratibu bonde la maji katika chanzo cha maji Mzakwe mkoani Dodoma kukutana  ofisini kwake siku  ya Jumatatu (kesho) pamoja na wajumbe zaidi ya 15 ili kuleta suluhu ya mgogoro huo ambao ni wa muda mrefu.

Aidha zaidi ya kaya 600 ziliondolewa katika hifadhi hiyo ambayo  Serikali imeweka mkakati  kabambe wa upandaji miti  katika eneo hilo.

Mtaka ambaye ambaye aliambatana na wataalamu wa mazingira katika ziara hiyo ameagiza taasisi hizo kuja na mpango kabambe wa kuanzisha uratibu wa maandalizi ya upandaji wa miti katika ekari 309  za mfano katika chanzo hicho cha maji ili kuweka mandhari nzuri ya Jiji la Dodoma.

"Wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo,jiji,pamoja na mamlaka ya bonde hili tunatakiwa kufanya maandalizi yatakayohusisha  utatuzi wa mgogoro ya wananchi kutoka maeneo yenye mgogoro,"amesema.

Nao baadhi ya viongozi ikiwemo kikosi cha kustawisha eneo la chanzo cha Maji Mzakwe wamesema watahakikisha wanatekeleza maagizo hayo katika kuhakikisha eneo hilo linakuwa la kijani .

Mtaalamu wa masuala ya mazingira kutoka chuo cha kilimo SUA Prof. Salim Maliondo amemhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kuwa kwa kutumia utaalamu wa Sayansi ya mimea,watalifanyia utafiti eneo hilo ili kubaini aina ya mití inayoweza kustawi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments