MASHINE YA MAJI YAENDESHWA KWA MAFUTA YA DIZELI MIAKA 8,TANESCO YAOMBWA KUPELEKA UMEME

Wananchi wa kijiji cha Karukekere wakichota maji

Na Dinna Maningo,Bunda 

WANANCHI wa Kijiji cha Karukekere kata ya Namhula wilaya ya Bunda mkoa wa Mara, wamesema kuwa ukosefu wa umeme kwenye mashine ya maji unawatesa, kwani wanalazimika kununua mafuta ya dizeli na kuyasafirisha kwa kutumia baiskeri mwendo wa kilomita 30 kupeleka kwenye mashine ya maji iliyopo ziwa Victoria.

Kutokana na changamoto ya umeme wameliomba Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka umeme ili mashine ijiendeshe kwa kutumia umeme badala ya kutumia dizeli kwakuwa umeme ulishafika kijijini na kwamba kijiji hicho kilijengewa mradi wa maji na halmashauri ya wilaya ya Bunda ulioanza kutoa huduma ya maji mwaka 2014 lakini mashine ya maji imekuwa ikisukumwa kwakutumia mafuta ya Dizeli jambo linalowapa usumbufu na kuwapotezea muda ambao wangeutumia kufanya shughuli zingine za kijamii.

Wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutembelea miradi ya maji katika wilaya hiyo,Fundi mradi wa maji wa karukekere,Kazi Kasuka alisema kuwa wakati wa msimu wa baridi mashine hutumia lita 20 za mafuta kwa siku na wakati wa kiangazi hutumia lita 40 kwa siku ambapo lita moja inauzwa sh.2571.

"Ndoo moja ya maji inauzwa sh. 50 kuna wengine wanalipa kwa bili kila mwezi,kuendesha mashine kwa kutumia mafuta ni gharama pesa inatumika nyingi inahitajika tupate umeme kupunguza gharama za matumizi,wananchi wanatumia baiskeri kuyasafirisha umbali wa,km 30 na njia siyo rafiki TANESCO itusaidie umeme", alisema Kasuka.

 Mhasibu wa kamati ya Jumuiya ya watumiaji wa maji,Jeremia Ngazi alisema kuwa mbali na changamoto hiyo ya ukosefu wa umeme,miundombinu ya mradi huo imezeeka na kujikuta wakitumia gharama za mara kwa mara kutengeneza miundombinu ya maji.

 "Miundombinu imechoka vifaa havidumu vinaharibika kila mara,havina uwezo wa kuhimili presha kwahiyo kila mara tunanunua vifaa,majuzi tumetengeneza laini mbili moja kwa gharama ya sh 30000 na nyingine sh 24000,tunapenda ikiwezekana serikali kupitia RUWASA watubadilishie miundombinu watuwekee mipya ambayo itakuwa imara kudumu kwa muda mrefu.

 " Kamati tuliomba RUWASA watupatie mabomba ya kuweka kwenye maeneo yenye changamoto,Meneja alituahidi kutupatia tunasubiri",alisema Jeremia.

Jeremia alieleza changamoto nyingine kuwa, baadhi ya watumiaji wa maji wanaolipa bili kwa mwezi huchelewa kulipa fedha nakurudosha nyuma utendaji wa kazi.

Hellena Paul muuzaji wa maji alisema kuwa mradi huo wa maji umekuwa mkombozi kwao kwani kabla yakuanzishwa akina mama walitembea umbali mrefu kwenda Ziwa Victoria kuchota maji,na kwa wale walioshindwa kutembea umbali mrefu waliyafuata kwa baiskeri na wengine kununua ndoo moja sh.500.

 "Tunahuduma ya maji lakini hayawekewi dawa mara kwa mara watu wanachota maji machafu yawekewe dawa kila mara",alisema Hellena.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Mwadawa Charles alisema kuwa kabla ya mradi huo walichota maji kwenye malambo ambayo nayo yalikauka wengine walifuata ziwani.

"Kule ziwani kulikuwa na changamoto ya watumiaji wa maji tukiingia tunakanyaga matope na kutoka nayo,tukiingia majini unapandisha nguo juu zisilowane unabaki uchi humo humo mnapishana na wanaume ambao nao wamefuata maji wanawake kwa wanaume walikuwa wanaoga ziwani maana kulikuwa na ka njia kadogo kalikoacha kwa ajili ya kupita wote tulipita hapo sasa maji tunayapata bombani tatizo ni umeme wa kusukuma mashine ndiyo hakuna", alisema.

Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Karukekere alisema kuwa kuwepo kwa mradi huo wa maji umesaidia wafike shule kwa wakati kwakuwa shule ina maji ya bomba.

Meneja Wakalama wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Bunda,William Boniface alisema kuwa mradi huo ulianza kutoa huduma ya maji 2014,ulighalimu Milioni 724 ulikuwa chini ya halmashauri ya wilaya ya Bunda.

Akizungumzia tatizo la ukosefu wa umeme uliosababisha mashine kuendeshwa kwa mafuta ya dizeli alisema kuwa alishalifatilia TANESCO ambapo kwa makadilio inahitajika kati ya Milioni 100-150 Kufikisha umeme kuliko na mashine ya kusukuma maji  na kuhusu ubovu wa mabomba alisema kuwa alishapewa taarifa ya changamoto nakwamba RUWASA itawapatia mabomba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments