RC HAPI AIPONGEZA TRA KUWAFUATA WAFANYABIASHARA KUWAELIMISHA KODI

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo (katikati) akizungumza wakati wa kikao cha kuhitimisha kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango kilichofanyika Musoma mjini mkoani Mara. Kampeni hiyo ilianza mkoani humo tarehe 7 na imemalizika leo tarehe 21 Februari, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Hapi akiwa katika picha ya pamoja na timu ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati walipomtembelea ofisini kwake kumpatia taarifa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango ambayo ilianza mkoani humo tarehe 7 na imemalizika leo tarehe 21 Februari, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Hapi akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Stephen Kauzen wakati timu ya maofisa wa TRA walipomtembelea ofisini kwake kumpatia taarifa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango ambayo ilianza mkoani humo tarehe 7 na imemalizika leo tarehe 21 Februari, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Hapi akizungumza na timu ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati walipomtembelea ofisini kwake kumpatia taarifa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango ambayo ambayo ilianza mkoani humo tarehe 7 na imemalizika leo tarehe 21 Februari, 2022. Kushoto ni kiongozi wa timu hiyo ambaye ni Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa Mamlaka hiyo Bw. Stephen Kauzeni.


Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Kilimo na Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mara Bw. Boniphace Ndengo (katikati) akizungumza wakati wa kikao cha kuhitimisha kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango kilichofanyika Musoma mjini mkoani Mara. Kampeni hiyo ilianza mkoani humo tarehe 7 na imemalizika leo tarehe 21 Februari, 2022.
Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Stephen Kauzeni akifurahia jambo na mfanyabiashara wa Msoma Mjini mkoani Mara Bi. Eunice Mmari wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango mkoani humo ambayo ilianza tarehe 7 na imemalizika leo tarehe 21 Februari, 2022.
Afisa Uhusiano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bi. Salome Mwandalanga akitoa elimu ya kodi kwa mfanyabiashara wa Musoma mjini mkoani Mara wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango mkoani humo ambayo ilianza tarehe 7 na imemalizika leo tarehe 21 Februari, 2022. (PICHA ZOTE NA TRA).

**************************

Na Mwandishi wetu
Musoma

Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ally Hapi ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuwafuata wafanyabiashara kwenye maeneo yao ya kazi ili kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi, hali itakayowajengea ari ya kulipa kodi kwa hiari.

Mhe. Hapi aliyasema hayo wakati timu ya maofisa wa TRA walipomtembelea ofisini kwake kumpatia taarifa ya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango ambayo imemalizika leo mkoani humo.

Alisema kuwa, kuna baadhi ya nchi wamefikia hatua anayegombea nafasi ya uongozi, historia yake ya ulipaji kodi inafuatiliwa na ikibainika aliwahi kukwepa kulipa kodi anapoteza sifa ya kugombea.

“Naamini kama nchi siku moja tufike mahali ambapo ili ugombee uongozi, historia nzuri ya ulipaji kodi iwe moja ya sifa, iwe fahari kuwa mimi ni mmoja wa walipakodi na ni sehemu ya maendeleo ya taifa,” alisema Mhe. Hapi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard Kayombo ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Mara, viongozi wa wafanyabiashara pamoja na wafanyabiashara wote kwa ushirikiano walioutoa kwa timu ya maofisa wa TRA waliofanya kampeni hiyo mkoani humo na kufanikisha kuwafikia jumla ya wafanyabiashara 4,014.

“Katika zoezi hili, tumefikia jumla ya wafanyabiashara 4,014 ambapo Wilaya ya Tarime tumefikia wafanyabiashara 2,088, Bunda 1,126 na Musoma mjini tumefikia wafanyabiashara 800,” Alieleza Bw. Kayombo.

Naye, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, Kilimo na Viwanda (TCCIA) Mkoa wa Mara Bw. Boniphace Ndengo ameishukuru TRA kwa kutoa elimu mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha mabadiliko ya sheria za kodi kila zinapopitishwa na Bunge.

“Niishukuru Idara ya elimu kwa mlipakodi, kazi mnayoifanya ya kutuelimisha ni kubwa sana. Moja ya eneo ambalo wafanyabishara tumekuwa tukilalamika ni kwamba sheria inapotungwa inaanza kutekelezwa mara moja lakini kwa sasa tunashukuru mnavyokuja kutupatia taarifa mapema ili na sisi tujipange vizuri,” Alisema Bw. Ndengo.

Wafanyabiashara wa Wilaya ya Musoma mkoani humo kwa nyakati tofauti wamesifia kitendo cha TRA kupita mlango kwa mlango kuwapatia elimu na kusema kwamba, wameepushwa na makosa yanayotokana na kutokuwa na uelewa wa masuala ya kodi.

Nyangaro Mseti ni mfanyabiashara wa Musoma mjini ambaye ameeleza kuwa, utaratibu huo unawasaidia kupata muda wa kutosha kuuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi kuhusu changamoto mbalimbali za kikodi zinazowakabiri.

Mfanyabiashara mwingine ni Eunice Julius, ambaye alisema awali walikuwa wakiitwa eneo moja kwa ajili ya kuelimishwa juu ya masuala mbalimbali ya kodi, lakini baadhi yao walikuwa hawaendi kwasababu walishindwa kufunga biashara wakihofia kukosa mauzo.

“Sasa mnatufuata na kutufundisha, akija mteja mnasubiri mpaka nimalize kumhudumia kisha mnaendelea, kwakweli utaratibu huu ni mzuri sana maana elimu tunapata na mauzo hayapungui ndiyo maana naomba muendelee tena mje mara kwa mara,” alisema Julius.
Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango mkoani mara ilianza tarehe 7 na imemalizika leo 21 Februari, 2022 ambapo timu ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania waliofanya kampeni hiyo wamefanikiwa kuwaelimisha wafanyabiashara wa Wilaya ya Tarime, Bunda na Musoma mjini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

1/Post a Comment/Comments

Post a Comment