WAMILIKI WA ARDHI WAPEWA SIKU 60 KUKAMILISHA KULIPA KODI YA PANGO LA ARDHI


Afisa ardhi mkuu , wizara ya ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi Biswalo Makwasa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuwajibika kulipa kodi huku akitoa Siku 60 kukamilisha zoezi hilo.
Mkuu wa kitengo cha kodi,Wizara ya ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi Denis Mesemu akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kuwakumbusha Watanzania kulipa kodi ya pango la ardhi Kwa mujibu wa sheria.

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA.

WIZARA ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi inawataka wamiliki wa ardhi kote nchini kujua wajibu wao kisheria wa kulipa kodi ya pango la ardhi  huku ikitoa siku 60 kwa wale ambao hawajalipa kodi hiyo na waliopimiwa viwanja kuwasilisha maombi ya kumilikishwa na wasipofanya hivyo  Serikali itachukua hatua za  kisheria.

Hayo yameelezwa leo 24 Februari,2022 na Afisa Ardhi Mkuu kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Biswalo Makwasa wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu umiliki ardhi kwa viwanja vilivyopimwa pamoja na ulipaji wa kodi ya pango la ardhi.

Amesema,wamiliki wa ardhi wanapaswa kujua wanawajibika kisheria kuwasilisha maombi ya kumikikishwa Ardhi kwa Kamishna wa Ardhi na kusisitiza kuwa kinyune na hapo itatolewa adhabu ya  kufuta umiliki,kupiga mnada na kumilikisha viwanja  vilivyopimwa kwa wananchi wengine wenye uhitaji.

“Wizara inatoa muda wa siku 60 kuanzia tarehe 5 mwezi wa pili 2022 ya kuhakikisha wale walipopimiwa viwanja wanawasilisha maombi  ya kumilikishwa  na wale wenye milki za ardhi wawe wamelipa kodi ya pango la ardhi,

Kila mmiliki wa ardhi anakumbushwa wajibu  wa kisheria kulipa kodi ya pango la ardhi,nisisitize TU kwamba zoezi la kufuta umiliki Kwa kutokidhi vigezo litaanza rasmi 6 Aprili,2022,"amesema

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Kodi,Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Denis Mesamu  ametoa rai kwa watanzania kulipa kodi ya pango la ardhi kwa njia ya kieletroniki kwa kutumia simu  kwani ni rahisi na ni rafiki.

Amesema ili kuboresha sekta hiyo,Serikali kupitia Wizara hiyo imefanya jitihada za kumfikia mwananchi moja kwa moja kupitia kituo cha huduma kwa wateja na kuondoa usumbufu wa ufuatiliaji wa masuala ya ardhi,kutunza kumbukumbu za wateja kielektroniki na kuwawezesha wananchi kupata taarifa zao kwa urahisi.

"Kodi ya pango la ardhi inakusanywa na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia mifumo ya Kieletroniki hivyo niwaombe wananchi wote wanaodaiwa kodi hiyo walipe kwa wakati kwani ni sheria na wajibu,"amesisitiza Mkuu huyo wa kitengo cha kodi,Wizara ya ardhi .

Licha ya juhudi hizo ameeleza kuwa bado kumekuwa na changamoto kwa watanzania kushindwa  kutofautisha kati ya  kodi ya pango la ardhi na kodi ya majengo  ambapo amesema kodi ya majengo  inakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwa sasa  inakusanywa kupitia luku kwenye umeme.

Akieleza mikakati ya Wizara hiyo amesema ina mkakati wa kwenda nyumba kwa nyumba kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinachodaiwa kinapelekewa hati ya madai ambapo amedai hali hiyo inaleta tija na hamasa.

"Kwa Mkoa wa Dodoma ulipaji wa kodi ya ardhi umeongezeka ambapo katika kipindi cha Disemba mwaka jana wiki mbili za kwanza ulipaji wa kodi ulikuwa wamiliki 200 lakini baada ya kuanza zoezi la kupeleka hati za madai walifika mpaka 800 kwa wiki na mapato yalitoka shilingi milioni 40 kwa wiki mpaka milioni 102,"amesisitiza.

Pamoja na mambo mengine ameeleza mipango endelevu ya ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi kwa mwaka na kueleza kuwa wamejiwekea malengo ya ukusanya shilingi bilioni 221 kwa mwaka ambapo makusanyo yaliyopo kwa sasa ni bilioni 81.2.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

1/Post a Comment/Comments

  1. WAPENI WANANCHI HATI ZAO WALIPE KODI YA ARDHI TATIZO NI NYINYI SERKALI KUWEKA MLOLONGO MREFU KUPATA HATI, HILO LIMEWAWEKA NJE WADAU WENGI, NAPESA ZINAPOTEA HAPP

    ReplyDelete

Post a Comment