WASINDIKAJI NA WAZALISHAJI WA MAZIWA WATAKIWA KUHAKIKISHA BIDHAA ZAO ZINAKUWA BORA

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto SSI.Mbarak Alhaji Batenga ( kati kati), Katibu Tawala Wilaya ya Kiteto Bw. Fadhili D. Alexander (Kushiro) na Meneja kanda ya Kaskazini (TBS) Bi Happy B. Kanyeka (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo kwa wasindikaji, wasambazaji na wauzaji wa maziwa na bidhaa za maziwa. Mafunzo haya yanalenga kuwaelimisha wadau wa maziwa kuhusu viwango vya maziwa na bidhaa za maziwa , utaratibu wa kuthibitisha ubora wa maziwa na bidhaa za maziwa, kanuni bora na taratibu za kusindindika maziwa na bidhaa za maziwa pamoja na kanuni bora za ufugaji.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Muhandisi Richard Runyango akifungua mafunzo kwa wasindikaji, wasambazaji na wauzaji wa maziwa na bidhaa za Maziwa wilayani Arumeru.
Mhe. Runyango aliwataka washiriki kuzingatia mada zote zinazotolewa na kuzifanyia kazi ili waweze kuzalisha Maziwa na bidhaa za Maziwa bora zitakazoweza kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Hai Bw. Yassin A Zayumba akifungua mafunzo kwa wasindikaji, wasambazaji na wauzaji wa Bidhaa za Maziwa wilayani Hai.
Maafisa wa TBS wakitoa mada kuhusu faida na matakwa ya kiwango cha maziwa na bidhaa za maziwa pamoja na kaununi bora za usindikaji, vifungashio na ufungashaji wa maziwa na bidhaa za maziwa . Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha washiriki kuboresha na kuongeza thamani katika mnyororo wa uzalishaji wa bidhaa husika na hatimae kuzalisha bidhaa bora na salama.

************************

Wajasiriamali wanaojishughulisha na ufugaji, ukusanyaji, ubebaji na usindikaji wa maziwa na bidhaa za maziwa wameshauriwa kuzalisha na kusindika maziwa yenye ubora ili kufanikisha azma ya Serikali ya kukuza sekta ya viwanda nchini.


Ushauri huo ulitolewa na Bi. Happy Kanyeka wakati wa mafunzo kwa wafugaji, wasindikaji, wasambazaji na wauzaji wa maziwa na bidhaa za maziwa yaliyofanyika katika wilaya za Kiteto (Manyara), Arumeru (Arusha) na Hai(Kilimanjaro)

Mafunzo hayo yamelenga kuwaelimisha wajasiriamali walio katika myororo wa thamani ya ufugaji, ukusanyaji wa maziwa ghafi, ubebaji na usindikaji wa maziwa na bidhaa za maziwa juu ya kanuni na matakwa ya msingi kuhusiana na shughuli wanazozifanya.

Akizungumza wakati wa mafunzo haya Bi Happy Kanyeka meneja wa kanda ya kaskazini (TBS) alisema, tunatambua kuwa sekta hii ya maziwa ina wajasiriamali wengi wadogo na wa kati ambao husindika na kupeleka sokoni maziwa na bidhaa za maziwa na walio wengi hufanya hivyo bila kufuata kanuni na taratibu zinazotakiwa hivyo kupelekea uwepo wa maziwa na bidhaa za maziwa hafifu sokoni pamoja na uharibifu na upotevu wa maziwa mengi sokoni.

“Kuna baadhi ya wasindikaji wa maziwa tayari walishaanza taratibu za kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ili kukidhi matakwa ya viwango husika lakini kutokana na changamoto za kukosa elimu juu ya viwango imepelekea mchakato wa uthibitishaji ubora kuonekana mgumu hivyo basi katika mafunzo haya tumeelekezana kuhusu kanuni bora za usindikaji, kanuni bora za ufungaji, kanuni bora za afya, faida na matakwa ya kiwango cha maziwa na bidhaa za maziwa pamoja na utaratibu wa kuthibitisha ubora wa maziwa na bidhaa za maziwa” ,aliongeza Bi Kanyeka.


Bi. kanyeka alisisitiza kuwa wilaya za Kiteto, Arumeru na Hai ni wilaya amabazo zinajihusisha na ufugaji wa ng’ombe wengi wakiwemo wa kienyeji na wa kisasa na usindikaji wa maziwa na bidhaa za maziwa ni moja ya shughuli inayofanya na wajasiriamali katika wilaya hizo.

“Mafunzo haya yametolewa katika maeneo muhimu sana yanayojishughulisha na Ufugaji wa Ng’ombe, usindikaji, usambazaji na uuzaji wa maziwa na bidaa za maziwa, pia ni azima ya serikali kukuza viwanda nchini endapo washiriki wa mafunzo haya watazingatia yale yote walioelekezwa taifa litakuwa na bidhaa bora na salama zitakazoweza kushindanishwa vyema katika sekta ya maziwa na bidhaa za maziwa ndani na nje ya nchi.”

Na katika kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi matarajio ya washiriki TBS imeshirikiana na taasisi nyingine ikiwemo SIDO, Bodi ya Maziwa (TDB) na TAMISEMI( ambao ni Afisa Afya, Afisa Mifungo, Afisa Biashara na Afisa Maendeleo ya Jamii)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post