SIMBA SC YAFUNGUA MWAKA MPYA 2022 KIBABE... YAIBAMIZA AZAM FC MABAO 2-1

Beki wa kulia wa Azam Fc Nicolas Wadada akijaribu kumtoroka kiungo mkabaji Raia wa Mali, Sadio Kanoute aliyefunga bao la kwanza katika mchezo wa Ligi kuu ya NBC Simba imeibuka na ushindi wa mabao 2-1.

************************

Na.Alex Sonna,Dar es Salaam

Mabingwa watetezi Simba wameanza vyema mwaka mpya kwa kusepa na pointi tatu dhidi ya matajiri wa Chamazi timu ya Azam FC baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mnamo dakika ya 13 Simba walikosa Mkwaju wa Penalti iliyochezwa na Rally Bwalya baada ya Frank Domayo kumchezea rafu ndani ya 18 winga Pape Sakho Penalti iliyondakwa na golikipa wa Azam Ahmed Salula.

Baada ya kukosa Penalti Simba waliendelea kulisakama lango la Azam FC kama nyuki mpaka zinaenda mapumziko hakuna timu iliyokuwa inamtambia mwenzie.

Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko mnamo dakika ya 67 kiungo Mkabaji Raia wa Mali, Sadio Kanoute alifunga bao la kwanza kwa kichwa na kuwanyanyua mashabiki wa Simba waliojitokeza katika uwanja wa Mkapa.

Licha ya kupata bao Simba waliendelea kulisakama lango la Azam na mnamo dakika ya 72 winga hatari kutoka Senegal Pape Sakho alipigilia msumari wa pili kwa bao safi la shuti kali lililomshinda mlinda mlango Salula.

Azam FC walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa mshambuliaji wao raia wa Zambia Rodgers Kola,akimalizia pasi ya Tepsi Evance.

Hadi mwamuzi Herry Sasii akipuliza kipyenga cha mwisho Simba wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kuondoka na Pointi 3 na kuendelea kuifukuzia Yanga kileleni Mwa Msimamo.

Kwa ushindi huo Simba wamefikisha Pointi 24 wakiwa nafasi ya pili wakiwa wamecheza mechi 10,Azam FC wanabaki nafasi ya tano kwa Pointi 15 huku Nafasi ya kwanza ikiendelea kushikiliwa na Yanga wenye pointi 29 wakiwa wamecheza mechi 11.

Simba na Azam FC wataelekea visiwani Zanzibar kushiriki Michuano ya Kombe la Mapinduzi linalotarajia kuanza kesho kwa mechi moja ya ufunguzi itakayowakutanisha Namungo FC.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments