SERIKALI YAAHIDI KUPITIA UPYA SHERIA,KANUNI NA SERA ZILIZOPITWA NA WAKATI KURAHISISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU TPC

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ,akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 28 wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kinachofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wizara ya Habari, mawasiliano na Teknolojia ya habari Dkt.Jim Yonazi akiongea kwenye mkutano Mkuu wa wafanyakazi wa shirika la posta nchini.

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog, DODOMA.

Serikali kupitia Wizara ya habari,Mawasiliano na Teknolojia ya habari imesema itapitia upya sheria,kanuni na sera zote zilizopitwa na wakati ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ndani ya shirika la Posta Tanzania(TPC).

Aidha imelielekeza Shirika hilo kuwa kinara na kuongoza jukumu la utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi linaloendelea nchi nzima


Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye wakati akifungua rasmi Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika hilo uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma leo.


Waziri huyo amesema,kuna baadhi ya sheria zimepitwa na wakati hali inayopelekea kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo hivyo kueleza kuwa ipo haja ya kufanya mabadiliko ili mambo mengine yaende.

Ili kuondokana na hayo Nape amesema Wizara yake itahakikisha inasimamia haki za watu kwa maslahi mapana ya Taifa na kupitia sheria kanuni na sera zilizopitwa na wakati ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kiutendaji.


Licha ya hayo Waziri Nape amesema kuwa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi utafanikisha na kuwezesha Posta ya Kidijitali na utendaji wa Shirika katika kuhudumia wateja na wananchi kwa ujumla na amewataka Mameneja wote wa TPC kushiriki kikamilifu katika jambo hili la anwani za makazi.

“Mameneja wa Mikoa yote wa Shirika la Posta Tanzania muwe wajumbe maalum na wa kudumu kwenye kamati ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima na muongoze utekelezaji wa jambo hili mikoa yote nchi nzima”, amesititiza Waziri Nape

Amewataka wajumbe wa Baraza la 28 la Mkutano huo kujadili kwa uwazi, kuambizana ukweli na kukosoana kwa staha ili kujenga umoja, kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika kwa kuwa anatambua kuwa uhai wa Shirika umebebwa na wafanyakazi wenyewe na Wizara itawasiliana na Wizara ya Fedha ya Mipango ili kufanikisha malipo ya deni la shilingi bilioni 26 kwa lengo la kuliondolea mzigo Shirika.

Akizungumza wakati akimkaribisha Waziri Nape, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa wateja wanataka kuona TPC ya kisasa inayofanana na mashirika mengine duniani na tayari TPC imeonesha taswira hii na Shirika linakua kiuchumi

“Wateja wetu cha kwanza anachokutana nacho siyo huduma unayompatia bali unavyompokea na kumhudumia, hivyo tuhudumie wateja wetu vizuri, tuipeleke mbele Serikali kwa kuwa tunawakilisha Serikali na tunafanya kazi kwa niaba ya Serikali,” amesisitiza Dkt. Yonazi

Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa TPC, Macrice Mbodo amesema kuwa katika mkutano huo, wajumbe watapatiwa mafunzo ya huduma kwa mteja; kupitia Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano (2022/33 – 2025/26) unaojikita kuifanya Posta ya Kidijitali kwa maendeleo endelevu; na kupitia bajeti na majukumu ya Shirika hilo kwa mwaka 2022/23.

Kwa upande wake Meneja wa TPC wa Mkoa wa Dodoma, Ferdinand Kabyemela amemshukuru Waziri Nape kwa kuwatengeneza huku akiahidi kuwa watafanya kazi kwa upendo ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika hilo.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments