TAKUKURU SHINYANGA : TUNATAKA MIRADI IWE NA THAMANI HALISI YA FEDHA ZINAZOTOLEWA


Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa akitoa taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU mkoani Shinyanga katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Oktoba – Desemba 2021) kwa waandishi wa habari leo Jumanne 25,2022
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa akitoa taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU mkoani Shinyanga katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Oktoba – Desemba 2021) kwa waandishi wa habari leo Jumanne 25,2022

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imesema itaendelea kufanya ufuatiliaji wa fedha zote za miradi ya maendeleo ikiwemo ya elimu na afya zilizotumika na zinazotarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na kukagua miradi yote inayotekelezwa ili kuhakikisha inakuwa na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na serikali ya awamu ya sita.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa leo Jumanne 25,2022 wakati akitoa taarifa ya kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU mkoani Shinyanga katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 (Oktoba – Desemba 2021).

“Tunataka kuhakikisha kuwa miradi inakuwa na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan”,amesema Mussa.

Akielezea kuhusu kazi zilizofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021, Mussa amesema walijikita katika kuzuia rushwa kwenye miradi ya maendeleo 62 inayotekelezwa mkoa mzima wa Shinyanga.

“TAKUKURU Shinyanga ilifuatilia miradi 62 yenye thamani ya shilingi 4,127,494,475/= kati ya miradi hiyo 62 miradi 60 ni miradi ya ujenzi wa madarasa yenye thamani shilingi 4,085,996,434/= inayotekelezwa katika halmashauri zote sita za mkoa wa Shinyanga. Miradi miwili ni ya rasilimali kilimo yenye thamani ya shilingi 41,498,041/= inayotelekezwa katika kata za Mwamalili na Pandagichiza wilayani Shinyanga”,ameeleza Mussa.


Amefafanua kuwa miradi hiyo 60 ni ya ujenzi wa madarasa yanayojengwa kwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambanao dhidi ya UVIKO – 19 ambapo miradi hiyo imekamilika na miradi miwili ya rasilimali kilimo inaendelea kutekelezwa.

“TAKUKURU Shinyanga ilifanya ufuatiliaji huo ili kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi hiyo zinatumika ipasavyo na miradi inakuwa na thamani halisi ikilinganishwa na fedha iliyotolewa. Lengo jingine ni kuhakikisha kuwa hakuna ubadhirifu wala ufujaji wa fedha”,amesema.

“Mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi wa miradi hii ambavyo yangeweza kusababisha mianya ya rushwa yamefanyiwa kazi kwa kufanya vikao na wadau ambao ni wasimamizi na watekelezaji wa miradi husika pamoja kutoa elimu kwa lengo la kuondoa mianya ya rushwa”,ameongeza.

Aidha amesema Ofisi ya TAKUKURU inaendelea na jukumu lake la kuelimisha umma huku ikitoa kipaumbele kuhamasisha wananchi wote kushirikiana na TAKUKURU katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Mkakati mkubwa kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2022 ni kuendelea kuto elimu kwa vijana wa Skauti ili waweze kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwajenga katika misingi ya kuwa waadilifu, wazalendo na wawajibikaji kwao na taifa lao. Pia washiriki kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kushiriki katika kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao”,amesema.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments