MAKAMU WA RAIS ATOA SIKU 7 KWA JESHI LA POLISI KUKAMATA WAHALIFU WA MAUAJI


Kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, na kulia ni Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango

Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 blog DODOMA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdory Mpango ametoa siku saba kuanzia leo kwa Jeshi la polisi nchini na idara zake zote kukamata wahalifu wa mauaji  yanayoendelea nchini na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Aidha ameliagiza Jeshi hilo kufanya kazi mchana na usiku kuwasaka na  kukamilisha uchunguzi wa matukio hayo ikiwa ni pamoja na vifo vya watu watano wa familia moja vilivyotokea katika Kijiji cha Zanka,Wilaya ya Bahi,mkoani Dodoma na kutaka taarifa hizo zipelekwe Ofisi ya Rais mara zitakapo kamilika.

Hatua hii imekuja kufuatia Watu watano wa familia moja akiwemo baba,mama,watoto wawili na mjukuu mmoja kukutwa wameuawa kinyama ndani ya nyumba yao Januari 22,2022 katika kijiji cha Nzaka, Wilayani Bahi Mkoani Dodoma jambo aliloliita ni ukatili unaoharibu taswira ya Jeshi hilo.

Akizungumza katika eneo lilipotokea tukio hilo ambapo alikwenda kuhani,Dkt. Mpango amesema,Serikali inasikitishwa na mauaji yanayoendelea nchini huku akitolea mfano matukio ya mauaji  yaliyoripotiwa hivi karibuni ya Mbeya,Mtwara na Kilimanjaro kuwa yanaitia doa Serikali.

"Nakuagiza kamanda wa polisi Mkoa wa Dodoma, fikisha salamu ya haya mauaji kwa  IGP Sirro,nataka haya mauaji tunayoyasikia kila siku yakome,mkahakikishe mnafanya kazi masaa 24 kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa,"amesema na kuongeza;

Jeshi la polisi mna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha amani inakuwepo,tumechoka hatuwezi  kuongoza nchi iliyojaa chuki na kuzaa mauaji ya kutisha,tunataka haya yasiyokee tena Katika Kijiji hiki cha Nzaka na sehemu zote nchini,"amesisitiza.

Makamu huyo wa Rais pia ameagiza Jeshi hilo kujichunguza Katika mifumo yake kutokana na kuhusishwa na baadhi ya matukio ya mauaji huku likikaa kimya bila kutolea ufafanuzi wa matukio hayo.

"Nimesikitishwa sana leo niliposikia kule Mtwara mtu ameuawa huku polisi wakihusishwa,ni dhambi sana ,tuwahurumie wananchi,tuwape amani,kunapokuwa na amani ndipo Maendeleo yanapatikana,"ameeleza .

Dkt. Mpango pia ameuagiza Uongozi wa Kijiji cha Zanka kufanya mikutano ya mara kwa mara ili kuhamasisha ulinzi ikiwa ni pamoja na kuhimizana kulindana.

"Haiwezekani watu wanakufa halafu majirani mpo na msijue,lazima kuna shida,miili ya marehemu inakaa siku tatu bila kutambuliwa na ndugu wala majirani wakati nyumba ziko karibu karibu sana,jambo hili linafikirisha sana,ifike mahali Kila mtu ajifunze kujua usalama wa jirani zake huo ndo utamaduni wa kitanzania,"amesisitiza .

Pamoja na hayo Dkt. Mpango ametumia nafasi hiyo kuwaasa viongozi wa dini nchini  kutumia nyumba za ibada   kuwakumbusha waamini wao kujua umuhimu wa upendo ikiwa ni pamoja na kulaani na kukemea mauaji yanayoendelea ya watu wasiokuwa na hatia.

Kumekuwa na matukio ya mauaji mara kwa mara nchini ambapo pia miaka mitatu iliyopita Katika Kijiji cha Zanka yalitokea mauaji baba na mama kuchinjwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments