MAKAMU WA RAIS AKERWA UCHAFU DODOMA


MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango leo tarehe 15 Januri 2022 ametembelea katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dodoma pamoja na Soko la Majengo kukagua utunzaji wa Mazingira katika maeneo hayo.

Akiwa katika mitaa hiyo Makamu wa Rais ameshuhudia uwepo wa takataka katika maeneo mbalimbali ambazo wananchi wamezikusanya lakini huchukua muda mrefu pasipo kuondolewa.


Wananchi hao wamemueleza Makamu wa Rais adha wanayoipata ya kuishi na takataka hizo jirani na maeneo yao kwa kipindi cha wiki mbili pasipo kuondolewa hali inayohatarisha usalama wa afya zao.

 Aidha wamesema licha ya kutoa fedha kwa mamlaka zinazokusanya takataka hizo lakini bado takataka hizo husalia katika maeneo yao ambayo pia hutumika kwa biashara za vyakula.

Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Dodoma mara baada ya kutembelea maeneo hayo, Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na hali ya usafi katika mkoa wa Dodoma.

Ameagiza kusimamishwa kwa mkataba baina ya Jiji la Dodoma na kampuni inayokusanya taka hizo (Green Waste) kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake kiufanisi.

Amewataka viongozi wa Jiji la Dodoma kuchukua hatua za haraka katika kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi pamoja na maeneo ya masoko na barabara zote.

Aidha Makamu wa Rais amewaagiza wakurugenzi katika maeneo mengine nchi nzima kuchukua zoezi la usafi kama zoezi endelevu na linapaswa kuzingatiwa kikamilifu.


Amewataka viongozi kuacha kukaa ofisini pekee bali pia kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo yao ili kufuatilia wale waliowapa dhamana ya uondoaji wa takataka hizo katika mitaa kama wanakidhi kuendelea kufanya kazi hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments