KAMATI ZA UKIMWI ZAAGIZWA KUKUTANA NA KUSHIRIKISHA WADAU MBALIMBALI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu Dkt. Pindi Chana akizungumza na Menejimenti ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (NGOME) jijini Dodoma Januari 26, 2022.

Mkurugenzi wa Mipango na Bajeti Bwa. Eleuter Kihwele akifafanua jambo katika kikao hicho.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu ( katikati) Mhe. Dkt. Balozi Pindi Chana , Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu ( wa kwanza kushoto) Mhe. Ummy Nderianga na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu wakifuatilia uwasilishaji wa Taarifa ya Uratibu wa Afua za Ukimwi Nchini kutoka TACAIDS katika kikao hicho


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu akifafanua jambo katika kikao hicho kilichofanyika pamoja na Menejimenti ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania.


Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania ( TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko akiwasilisha Taarifa ya Uratibu wa Afua za Ukimwi Nchini katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania ( TACAIDS) wakifuatilia kikao kilichofanyika kati ya tume hiyo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Dkt. Balozi Pindi Chana Jijini Dodoma.

************************

Na Mwandishi Wetu- Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. . Pindi Chana,ameagiza kamati za UKIMWI za ngazi ya Kata,Wilaya na Mkoa kuendelea kukutana na kufanya majadiliano kuhusu masuala ya Mwitikio wa UKIMWI nchini kwakuwa kamati hizo zipo kimuundo.

Mhe. Pindi alizungumza hayo Januari 26, 2022 Jijini Dodoma alipokutana na Menejimenti ya Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa lengo la kupata uelewa kuhusu muundo,na majukumu yanayotekelezwa na tume hiyo ikiwa ni mwendelezo wa kukutana na taasisi zote zilipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu .

Alisisitiza kuwa iwapo kamati hizo zitakaa na kujadili masuala ya UKIMWI na kushirikisha wadau wengine itasaidia katika kuongeza uelewa wa namna ya kupunguza maabukizi mapya ya VVU.

“Nitumie nafasi hii kuomba kamati za UKIMWI ngazi ya Wilaya , Kata na Mkoa, kamati hizi zipo kimuundo ziendelee kukutana na kujadili masuala mbalimbali jinsi gani tunaweza tukadhibiti suala hili zima la UKIMWI na hatimaye tupate Taifa ambalo liko huru dhidi ya maambukizi haya na virusi hivi vya UKIMWI,” alisema Waziri Pindi.

Vile vile alitoa wito kwa watanzania kujitokeza kupima afya ili kufahamu hali zao mapema na kujua haua za kuchukua ili kujikinga kutopata maambukizi mapya na kuambukiza wengine Pamoja na kuanza matumizi ya ARV kuimarisha afya zao ili kuendelea kushiriki shughuli za kiuchumi.

“Nitoe wito kwa watanzania wengi ni muhimu sasa tuanze kupima na kuzijua afya zetu ili kuweza kudhibiti, maana unapojijua afya yako iko vipi inakuwa rahisi sana kuepukana na maambukizi mapya ya VVU,” alieleza Mhe. Pindi.

Hata hivyo alipongeza hatua za TACAIDS kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na maambukizi ya VVU kupitia njia mbalimbali hatua iliyochangia kupungua kwa maambukizi mapya na vifo vitokanavyo na UKIMWI .

Aidha alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kuhakikisha mapambano dhidi ya virusi hivyo yanafanikiwa huku akimpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kuwa balozi mwema katika mapambano hayo.

Akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya TACAIDS, Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Leonard Maboko alibainisha kwamba kiwango cha upimaji wa VVU kimeongezeka kutoka asilimia 61 ya makadrio ya watu wanaoishi na VVU mwaka 2016 hadi asilimia 81.1 mwaka 2020.

Pia Matumizi ya dawa za kufubaza VVU (ARV) kwa WAVIU wanaojua hali zao za maambukizi yameongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi 98.3 mwaka 2020 wakati kiwango cha kufubaza VVU kwa wale wanaotumia ARV kikiongezeka kutoka asilimia 87 mwaka 2016 hadi asilimia 95.1 mwaka 2020.

vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 50 kutoka 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020. Maambukizi mapya ya VVU kwa watu wazima miaka 15 na zaidi yameshuka kutoka 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020 Maambukizi mapya kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto yameshuka kutoka 18% mwaka 2010 hadi 7% mwaka 2020.

Katika hatua nyigine Dkt. Maboko ameainisha maeneo ya kuongeza nguvu katika mwitikio wa UKIMWI kuwa ni Kuzuia maambukizi mapya ya VVU - hasa kwa Vijana kwani zaidi ya theluthi moja ya maambukizi mapya hutokea kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24, hususan vijana wa kike, kuzuia maambukizi mapya ya VVU na kuimarisha huduma za upimaji na matumizi ya ARV kwa makundi maalum, kama vile Wavuvi, madereva wa masafa marefu, wachimbaji katika migodi, wanaifanya kazi za kuhama hama kama wakulima katika mashamba makubwa, wafanyakazi katika miradi mikubwa ya ujenzi na wanaofanya biashara ya ngono.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu, alifafanua kwamba bado kuna jitihada zinahitajika kuhakikisha rasimali za mfuko wa udhamini wa kudhibiti UKIMWI (ATF)zinapatikana hasa kuwa na vyanzo vya uhakika vya ndani vya mfuko huo.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments