THRDC YAPAZA SAUTI KUHUSU MGOGORO WA ARDHI WILAYANI NGORONGORO


Mratibu wa Kitaifa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa wakati akizungumza na wanahabari akitoa taarifa ya hali ya utetezi wa Haki za Binadamu katika migogoro ya Ardhi Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha
Wakili kutoka THRDC Lulu Maro akitoa taarifa ya ya hali ya utetezi wa Haki za Binadamu katika migogoro ya Ardhi Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha
.....................................      

NA MUSSA KHALID,DAR ES SALAAM

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluh Hassan kuwapa nafasi na kuwasikiliza wananchi wa Loliondo ili kusikia hoja zao na hatimaye azifanyie kazi ili kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu.

Kauli hiyo imetolea leo Jijini Dar es salaam na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC Onesmo Olengurumwa wakati akizungumza na wanahabari akitoa taarifa ya hali ya utetezi wa Haki za Binadamu katika migogoro ya Ardhi Wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Olengurumwa amesema Wilaya ya Ngorongoro ina jumla ya Kilomita za mraba zaidi ya 14,ambapo zaidi ya asilimia 75% ya eneo hilo kwa sasa hutumika kwa shughuli za utalii na uhifadhi lakini pia kilomita za mraba 4000 kwa sasa zimebaki kwa matumizi ya makazi ya watu na shughuli za kijamii.

‘Taharuki imekuwa ikiibuka mara kwa mara katika kipindi cha miaka toka mwaka 1992 matukio ya kuhamishwa watu yamekuwa yakifanyika mara ka mara na huku ukiukwaji wa haki za binadamu ukishuhudiwa hivyo kwa sasa tunaamini Mhe Rais Samia akitoa nafasi ya kuwasikiliza wananchi wa Ngorongoro huenda akawa ni wa kwanza kupatia ufumbuzi wa kudumu migogoro ya ardhi na uhifadhi Wilayani Ngorongoro’amesema Olengurumwa

Aidha ameiomba serikali kusitisha mpango wake wa kuchukua ardhi za vijiji na badala yake ikae na wananchi ili kutafuta suluhu itakayokubaliwa na pande zote.

Vilevile ameiomba Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko ya wananchi na kuchukua hatua stahiki ili kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu Wilayani Ngorongoro.

Katika hatua nyingine amewataka wananchi wa Loliondo kuwa tayari kukaa mezani kwa lengo la kujadili suluhu ya kudumu kwa manufaa ya pande zote mbili ikiwa ni pamoja na haki zao pamoja nha shughuli za uhifadhi kwa maslahi ya Taifa.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wa Watetezi wa Haki za Binadamu na Azaki wa Haki za wafugaji Wakili kutoka THRDC Lulu Maro amesema kuwa wanasikitiswa na ushiriki mdogo wa mashirika ya haki za binadamu katika kufanya utetezi kuhusuana na mgogoro huo na hivyo kufanya haki za wananchi kupotea ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Amesema ni vyema viongozi wa juu wa serikali wakaacha kukaa kimya badala yake wafanye jitihada za kuwasikiliza wananchi wa Loliondo,Ngorongoro ili kuwafanya wananchi wasiichi maisha ya hofu muda wote.

Hata hivyo washirika wa Kimataifa na wadau wa maendeleo wameombwa kuendelea kuwasaidia watetezi wa Haki za Binadamu na serikali kutafuta njia bora naya kudumu ya kutatua migogoro hiyo kwa maslahi ya pande zote mbili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments