SERIKALI KUPELEKA HUDUMA ZA KIBINGWA KWENYE MAKAO YA WAZEE NA WATOTO

Waziri wa Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi maalumu Dkt.Dorothy Gwajima akiongea Katika kituo cha makao ya watoto Hombolo Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi maalumu Dkt. Zainab Chaula akiongea na wadau huku akihamasisha kuwa jukumu la kila mwananchi ni kusaidia kuchochea hamasa ya maendeleo na kuachana na utegemezi.

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 blog, DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia ,wanawake na makundi maalumu imesema inafikiria kuwasiliana na Wizara ya Afya kuona haja ya kupelekea madaktari bingwa katika vituo vya makao ya Wazee na Watoto nchini ili kuwapatia huduma za kiafya kwa wagonjwa wenye magonjwa ya kibingwa na msaada wa kisaikolojia ,marekebisho ya tabia, unasihi na msaada wa kisaikolojia na kijamii.

Hatua hii imekuja kufuatia Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo Dkt. Dorothy Gwajima kufanya ziara leo katika kituo cha makao ya Wazee na Watoto cha Mtakatifu Teresa,Hombolo Jijini Dodoma(Home of Love and joy)kujionea baadhi ya Wazee Wana magonjwa yanayohitaji huduma za kibingwa.

Dkt. Gwajima amesema huduma hiyo itasaidia kuwaondolea usumbufu wagonjwa na wanaowahudumia hasa kutokana na baadhi ya huduma hizo kupatikana kwa umbali mrefu na kuwa usumbufu kwao kutokana na umri.

Amesema changamoto nyingi zilizopo kwenye vituo vya malezi zinahitaji nguvu ya upendo ndiyo maana Serikali na Wadau wake inaendelea kutekeleza mambo mengi ikiwemo kuwezesha watoto 5,390 waliotambuliwa kuwa wanaishi na kufanya kazi mitaani ambao kati yao 135 waliunganishwa na familia zao huku 821 wakipatiwa vifaa vya shule na 75 familia zao ziliunganishwa na huduma za kuimarisha uchumi wa kaya.

Dkt. Gwajima pia ameeleza vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na watoto wachanga 303 vikiwa na idadi ya watoto 6,772 vilisajiliwa na hivyo kufanya idadi ya vituo kufikia 2,068 vyenye jumla ya watoto 163,394 walioandikishwa nchi nzima ikiwa ni pamoja na nyumba Salama Sita (6) kusajiliwa za hifadhi ya muda kwa waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

"Serikali imefanikisha kusajili makao 24 ya Kulelea Watoto Wanaoishi katika Mazingira Hatarishi yenye watoto 707 hivyo kufanya idadi ya Makao kuwa 244 yenye idadi ya watoto 24,254 nchini pamoja na huduma kwa watoto 116 wanaokinzana na sheria ambapo 58 wanahudumiwa katika Mahabusu 5 za Watoto na 58 wanapatiwa huduma ya marekebisho ya tabia katika Shule ya Maadilisho Irambo-Mbeya",amesema.

Ameeleza kuwa jumla ya mashauri ya jinai 188 yamefanyiwa kazi yanayohusisha watoto 229 waliopatiwa msaada wa kisheria, marekebisho ya tabia, unasihi na msaada wa kisaikolojia na kijamii.

Katika kuhakikisha kuwa kipindi cha utoto kikiisha mtoto hapotezi dira ya maendeleo, Aprili 17, 2021 Serikali ilizindua Agenda ya Kitaifa ya kuwekeza kwenye Afya na Maendeleo ya Vijana Balehe.

Licha ya kazi hiyo kubwa, bado kuna watoto wengi wanaoishi kwenye mazingira hatarishi (mitaani) hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau wake inaendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo hasa ikizingatiwa kwamba takwimu zinaonesha waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili kwa upande wa watoto 70% ni wa kike.

"Pamoja na serikali na wadau wake kuendelea kupambana kuzuia ukatili pia inatoa huduma kwa wahanga wa ukatili ikiwemo huduma ya kisheria ambapo kwa mwaka 2020/21 mashauri 3889 yamepelekwa Mahakamani na 1,504 yametolewa hukumu na mengine kazi inaendelea;

Ukiacha ukatili kwa watoto hata watu wazima wanafanyiwa ukatili ambapo wanawake wanatengeneza 96% ya wanaoathirika, ukatili kwa mtu yeyote haukubaliki, hivyo serikali itaendelea kuimarisha utekelezaji wa afua zenye kuhamasisha kuzuia na kushughulikia aina zote za ukatili ili kuhakikisha jamii ya kitanzania inafurahia haki ya kuishi,"amesisitiza.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema ili kuondokana na matatizo kwa Wazee na Watoto ni jukumu la kila mwananchi kusaidia kuchochea hamasa ya maendeleo huku akitolea mfano wa bwawa la Hombolo kutumika kama kichocheo cha shughuli za uchumi.

Amesema,Serikali kwa upande wake itahakikisha ustawi wa jamii kwa wazee waliotambuliwa kuwa hawajiwezi ambapo wameendelea kutunzwa kwenye makao 13 ya serikali ya wazee pamoja na makao mengine ya watu na taasisi binafsi mfano hapa Hombolo.

"Lazima kila mtu awajibike kwa nafasi yake kuhakikisha hakuna madhara kwa Wazee wala watoto, hitaji kubwa la wazee ni kuimarisha huduma zao muhimu,watu hawa wanatutegemea sisi tusipofanya kazi kwa bidii tunahatarisha pia usalama wao,"amefafanua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments