BODI YA FILAMU YAWATAKA WADAU KWENDA NA TEKNOLOJIA


Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo akifafanua masuala ya tasnia ya Filamu wakati wa kikao na wadau wa tasnia ya Filamu , Viwanja vya Chinangali park Jijini Dodoma.


Afisa Maendeleo ya Filamu Happy Maduhu akieleza jambo wakati wa kikao na wadau wa tasnia ya Filamu , Viwanja vya Chinangali park Jijini Dodoma


Gosbert Mvungi moja ya Mzalishaji wa kazi za Filamu wakati wa kikao na wadau wa tasnia ya Filamu , Viwanja vya Chinangali park Jijini Dodoma

........................................................

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo amewataka wadau wa Tasnia ya Filamu kutumia fursa za teknolojia ili kuongeza wigo wa masoko ya kazi za Filamu kwa lengo la kujiongezea kipato na manufaa kwa jamii.

Ameyasema hayo wakati akiongea na wadau wa tasnia ya Filamu wakiwemo wazalishaji, waigizaji, waandishi wa miswada ya Filamu wa Jiji la Dodoma Januari 25,2022 katika Viwanja vya Chinangali Park, Jijini hapo.

Akifafanua kuhusu suala la matumizi ya Teknolojia katibu amebainisha kuwa ili kazi za Filamu ziweze kuwafikia watu wengi na kuwa na manufaa makubwa kwa wanatasnia ni vyema kujielekeza katika kupeleka kazi hizo kwenye vingamuzi vya Televisheni zenye Chaneli za Filamu, matumizi ya mitandao ya kijamii kama Youtube na mitandao mingine. Jambo ambalo linaongeza tija ya usambazaji wa kazi hizo kwa urahisi tofauti na hali ilivyokuwa awali.

“Nitoe rai kwenu kwamba tusibaki nyuma katika matumizi ya Teknolojia, twende na kasi ya teknolojia Pamoja na kuongeza ubunifu katika kazi zetu ili twende na kasi ya ushindani wa dunia,” alisema Dkt. Kilonzo

Aidha, Katibu amesema miongoni mwa mikakati mahususi ya Bodi ya Filamu katika kuweka mazingira wezeshi kwa wanatasnia ya Filamu wa mikoa yote ili kuweza kufikia malengo yao ni pamoja na kuendelea na mradi wa kurasimisha Vibanda Umiza kupitia maafisa Utamaduni wa mikoa. Vilevile Bodi kuendelea kutoa mafunzo kwa wadau ili kuboresha na kuinua tasnia ya Filamu nchini.

Sambamba na mikakati hiyo, ilielezwa kuwa Bodi itaendelea kushirikiana na kutoa tuzo mbalimbali za kutambua utendaji mzuri wa wanatasnia kwa lengo la kuwaongezea ari na motisha ya kazi za Filamu.

Kwa upande wake mzalishaji wa kazi za Filamu Bw. Gosbert Mvungi ameshauri Bodi kuendelea kutafuta fursa za wawekezaji kuwekeza katika Tasnia ya Filamu hasa katika masoko ya Televisheni kwaajili ya kazi za Wanatasnia. Jambo ambalo litaongeza fursa ya kuwainua na kuwaendeleza tasnia ya Filamu nchini.

Pamoja na mambo mengine wadau hao wamebainisha kuwa matumizi ya lugha ya Kiswahili ni moja ya suala muhimu linalosaidia uuzaji mzuri wa Filamu za Kitanzania na kuwezesha Filamu hizo kushika nafasi bora kitaifa na Kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments