MWANAJESHI ADAIWA KUMUUA BABA YAKE MZAZI KWA KUMCHINJA AKIMTUHUMU NI MCHAWI MBEYA

JESHI la Polisi mkoani Mbeya limethibitisha kutokea mauaji ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Edward Ndonde anayedaiwa kuuawa kikatili kwa kuchomwa visu na mtoto wake, Mussa ambaye ni mtumishi wa Ruvu JKT.

Mussa anadaiwa kufanya mauaji hayo jana Jumatano Januari 12, 2022 nyumbani kwa baba yake mtaa wa Lumbira Kata ya Iwambi jijini Mbeya.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Christina Musyani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa chanzo ni kutuhumiana kwa mambo ya kishirikina.

Amesema mtuhumiwa ambaye ni mtumishi wa Ruvu JKT amekamatwa baada ya kufanya mauaji hayo na kwamba uchunguzi unaendelea ili hatua za kisheria ziweze kushika mkondo wake.

“Ni kweli tukio lipo na limetokea leo, ambapo pia marehemu alikuwa mwalimu mstaafu, chanzo kinadaiwa kuwa mambo ya kishirikina, ambapo mtuhumiwa alikuwa anamtuhumu baba yake kuwa ni mchawi na Jeshi la Polisi limemshikilia kwa uchunguzi zaidi,” amesema Christina.

Balozi wa mtaa huo, Hezron Thobias amesema baada ya tukio hilo mtuhumiwa alianza kutamka maneno kuwa amemaliza kazi yake aliyoitiwa na baba yake ya kuchinja kuku, jambo lililowashtua na kwenda kuangalia waliposikia kelele zikitoka ndani.

“Alionekana kama ana ugoro na amelewa, akawa anatamka maneno kuwa amemaliza kuchinja kuku, tukamuona mama yake analia anasema njooni muone mtoto alichofanya akiwa anatokwa machozi, ile tunaingia ndani tukakuta amemuua, damu zimemwagika,” amesema Thobias.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Alhaji Saad Kusilawe amesema marehemu aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi Taifa ambapo alikitumikia kwa muda wote kwa uadirifu na kwamba wanasubiri maelekezo kwa ajili ya taratibu za mazishi.

“Tumepoteza hazina ya kiongozi, kwani katika utumishi wake aliweza kumaliza vyema hadi anastaafu, ni pigo kubwa na ni masikitiko makubwa,” amesema Kusilawe.

 ******

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia MUSSA EDWARD NDONDE @ SANGA MAPESA [31] Askari wa JWTZ MT.109772 Kikosi cha Ruvu JKT mkoani Pwani na Mkazi wa Mlandizi kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi aitwaye EDWARD NDONDE [75] Mwalimu Mstafuu, Mkazi wa Lumbila Jijini Mbeya kwa kumkatakata visu sehemu mbalimbali za mwili wake.  

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 12.01.2022 majira ya saa 09:00 asubuhi huko Mtaa wa Lumbila uliopo Kata ya Iwambi, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya ambapo mtuhumiwa aliuawa EDWARD NDONDE [75] ambaye ni baba yake mzazi kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na kisha kumkata kiganja cha mkono.

Chanzo cha tukio ni tuhuma za ushirikina kwani inaelezwa kuwa mtuhumiwa anadai kuwa marehemu ambaye ni baba yake mzazi ni mchawi anamloga ili hasifanikiwe kwenye mambo yake. Awali  mtuhumiwa alifika nyumbani kwa marehemu majira ya 09:00 asubuhi pasipo kutoa taarifa  yoyote ya  kuja Mbeya na kuingia moja kwa moja sebuleni na kuanza kumshambulia kwa kisu na stuli na kupelekea kifo chake.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa uchunguzi wa kitabibu. Mtuhumiwa anaendelea kupatiwa matibabu chini ya ulinzi Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya baada kushambuliwa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi kutokana na tukio alilofanya. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linalaani tukio hili baya kutokea na litahakikisha mtuhumiwa anafikishwa kwenye mamlaka husika ya sheria kwa hatua zaidi. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa rai kwa wananchi kuachana na Imani potofu za kishirikina hasa kuamini waganga wapiga ramli chonganishi kwani ni hatari kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa. 

Imetolewa na:

[CHRISTINA A. MUSYANI – ACP]

KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments