WAHITIMU SJUT WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI NA KUTENDA HAKI KWA JAMII


Na Dotto Kwilasa, Dodoma

MAKAMU Mkuu wa Chuo kikuu cha St. John's Tanzania (SJUT) Prof. Yohana Msanjila amewataka wanafunzi wanaomaliza muda wao wa masomo chuoni hapo kuzingatia maadili na kutenda haki kwa jamii kupitia taaluma zao.

Amesema hayó mwishoni mwa wiki hii jijini Dodoma katika mahafali ya 12 ya chuo hicho ambapo jumla ya wanafunzi 1248 walitunukiwa vyetu kwa ngazi ya Astashahada,Stashahada ,Shahada na Shahada za uzamili.

Prof. Msanjila amewaambia wanafunzi hao kuwa elimu waliyoipata chuoni hapo ni vema wakaitumia kuleta Maendeleo ya taifa na kwamba kwa kufanya hivyo itakuwa ni sifa nzuri kwa chuo hicho ambacho kinaendana na maadili ya dini.

"Nina furaha kwa kuwa mmemaliza salama,matumaini yangu ni kwamba huko muendako hamuendi kutuaibisha ,hakikisheni mnakumbuka kuitumia elimu nzuri tuliyowatunuku kwa jamii na kukumbuka kwamba ni vema kutoa kuliko kupokea,"amesema Makamu mkuu huyo wa SJUT.

Aidha Prof. Msanjila amesema taswira nzima ya chuo hicho inategemea ubora wa huduma watakayo itoa kwenye jamii katika masuala ya Afya,elimu,Sheria na mengineyo na hivyo kuwataka kupeperusha bendera hiyo kwa kuwa mfano mzuri nchini na duniani kote.


"Mkitenda haki hata jamii itawashukuru na hii ndiyo ahadi mliyoitoa kwenye viapo vyenu kwamba mnaenda kulitumikia taifa kwa moyo wa dhati bila upendeleo wowote na wala kumuonea mtu yoyote,elimu hii ni kichocheo cha ajira na ujasiriamali msiende kujibweteka,"amesisitiza.


Sambamba na hayo amesema kwa zaidi ya miaka 14 chuo hicho kimetengeneza wanafalsafa ,watafiti,wajasiriamali na viongozi mashuhuri na kwamba tunuku hizo ni faida kubwa kwa chuo hicho kwa kuwa inadhihirisha mafanikio .

Naye Mkuu wa Chuo hicho Askofu Mkuu Mstaafu Donald Leo Mtetemela ameeleza kuwa Dodoma ni Jiji linalokua kwa kasi hivyo chuo hicho kinajivunia kuwa sehemu ya ukuaji huo na kuendeleza ushirikiano na vyuo vyote vya elimu ya juu na vya kati.


Katika ujumbe wake alioutoa kwenye hafla ya mahafali hiyo,Askofu huyo amesema"Wahitimu wetu wameenea maeneo mbalimbali,kama Taasisi tunafurahi wakati wote na kuwaombea muwajibike ipasavyo Kwa kuzingatia maadili ya utu wa mtu,"amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho (SJUT) Prof. Penina Mlama amesema chuo hicho tangu kimeanzishwa wanafunzi zaidi ya elfu 15 wamehitimu huku akieleza kuwa mchango wa wahitimu wote unaendelea kuboresha hali ya maisha ya watanzania.

Amesema,tangu kuanza kwa chuo hicho, kimefanikisha kuanzisha programu nyingi zikiwemo shahada ya Sanaa na elimu,astashahada ya kilimo,stashahada ya Sheria,shahada ya Benki na fedha,shahada ya uuguzi,shahada ya famasi,shahada ya uzamivu na nyingine nyingi.

"Mwaka huu ni mwaka wa mafanikio kwetu kwa kuwa kati ya wahitimu 1248 ,551 kati yao ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 44.2 huku wanaume wakiwa na idadi ya 697 sawa na asilimia 55.8,tunaendeleza zaidi juhudi za kuwawezesha wanawake kupenda kujiendeleza,"amesisitiza.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamepelekea kupata ithibati ya Tume ya vyuo vikuu (TCU) kwa Miaka na kidhihirisha kuwa elimu inayotolewa hapo inakidhi viwango vya kimataifa.

Aidha amesema katika kuendeleza ari ya kutoa elimu ya viwango vya juu,Chuo hicho kupitia kada ya Sayansi wamenza mchakato wa kuengeneza chanjo ya korona ikiwa ni pamoja na kuboresha maabara za kemia na kuwapa fursa wanafunzi kufanya mazoezi kwa vitendo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments