NAIBU WAZIRI MAMBO YA NJE AFANYA ZIARA EXPO 2020 DUBAI - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Sunday, December 19, 2021

NAIBU WAZIRI MAMBO YA NJE AFANYA ZIARA EXPO 2020 DUBAI


*************************

Na Abubakari W Kafumba na Happiness Shayo,UAE

Leo tarehe 19 Desemba, 2021 Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai Mhe. Balozi Mohamed Mtonga na Mkurugenzi wa banda hilo Bi. Getrude Ng’weshemi kutoka TanTrade, wamemkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na ujumbe wake.

Mara alipowasilili, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alifanya kikao kifupi na watumishi wanaoziwakilisha Taasisi za Sekta mbalimbali nchini Tanzania zinazoshiriki kwenye Maonesho ya Dunia ya Expo 2020 Dubai ambapo alipokea taarifa iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania, Bi. Getrude Ng’weshemi inayohusu ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai ikiainisha mafanikio yaliyopatikana, jinsi sekta mbalimbali zinavyoitangaza Tanzania kwenye maonyesho hayo na hatua zinazochukuliwa ili kuhakikisha ushiriki unaendelea kuwa wa uhakika na wenye tija.

Aidha Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ametumia fursa hiyo kuhimiza ushiriki wenye tija na wa uhakika utakaoipa nchi hadhi inayostahili na hatimaye kufikia malengo makuu ya kitaifa ya ushiriki kwenye maonyesho haya kama ilivyopangwa.

Vilevile amechukua nafasi hiyo kushauri namna bora ya kuandaa ‘Tanzania National Day’. Amesema,” Tujifunze kutoka kwa wenzetu ambao walishaandaa shughuli zao ili ya kwetu iwe ya aina yake. Tujipange na tujiandae vema ili tuhakikishe siku hiyo Tanzania inapata heshima yake. Kati ya nchi 192, tumepewa heshima ya kuwa miongoni mwa mataifa makubwa ulimwenguni kuwapo hapa leo. Tuitumie nafasi hii kujijengea jina kubwa zaidi na kuonyesha fursa zinazoiweka Tanzania mbele kama moja ya nchi yenye maendeleo ya kasi. Tunategemea maonyesho haya ni yataleta manufaa kwa Tanzania na watanzania”.

Hii ni sehemu nzuri ya kujifunza, kupata uzoefu, kujitangaza, kuleta hamasa kubwa na kuchochea ukuaji na maendeleo ya Sekta mbalimbali kupitia mafanikio ya ushiriki wa Tanzania kwenye maonyesho haya ikiwemo uwekezaji wa kisekta na ushirikiano endelevu baina ya Tanzania na mataifa mengine ulimwenguni.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages