AUAWA AKIJARIBU KUGUSA UPANGA MAALUM NDANI YA HEKALU LA DHAHABU


Hekalu la dhahabu
 **
Polisi katika mji wa Amritsar nchini India wamesema kuwa mwanaume mmoja anayeshukiwa kujaribu kufanya kitendo cha kufuru katika hekalu takatifu la Sikhism amepigwa hadi kufa.

Kisa hicho kilitokea wakati wa ibada ya maombi kwenye Hekalu la dhahabu la jiji hilo siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya eneo hilo.

Mwanaume huyo anadaiwa kujipenyeza kwenye ukumbi wa ndani, ambapo kitabu kitakatifu cha Guru Granth Sahib, kinawekwa.

Kisha akajaribu kugusa upanga maalum uliowekwa karibu na kitabu, lakini alizidiwa nguvu na walinzi na waabudu.

Mzozo huo ulifanyika mwendo wa kumi na mbili kasoro saa za huko na alinaswa na kamera huku maombi ya jioni yalipokuwa yakitangazwa kwenye televisheni.

Haijulikani ni nini hasa kilitokea baadaye. Polisi walisema mtu huyo alipatikana akiwa amefariki mara tu maafisa walipofika eneo la tukio, na uchunguzi unaendelea.

Katika ujumbe wa Twitter, Waziri Mkuu wa Punjab Charanjit Singh Channi alisema aliamuru polisi "kuchunguza chanzo cha tukio hilo kutisha".

Tukio hilo linajiri siku chache baada ya mwanaume mwingine kukamatwa kwa madai ya kutupa kitabu kitakatifu cha Sikh, Gutka Sahib, kwenye kisima cha maji kilichotengenezwa na mwanadamu kuzunguka hekalu hilo.

Kudhalilishwa kwa Guru Granth Sahib ni suala la kuhuzunisha sana miongoni mwa jamii ya Sikh.

Udhalilishaji kadhaa ulifanyika mnamo 2014 na 2015, na ikawa suala kuu la kisiasa wakati wa uchaguzi wa Punjab mnamo 2017 na 2019.

Chama tawala cha Congress kilishutumiwa na wapinzani wa kisiasa, kwa kushindwa kuleta haki kwa wahalifu waliopita wa kunajisi.


Balwinder Bhunder, mbunge wa chama cha upinzani Akali Dal, alilaani tukio la hivi punde siku ya Jumamosi, akiambia chombo cha habari cha NDTV kwamba lilikuwa ni jaribio la makusudi "kudhoofisha Punjab, ambayo ni mkono wa upanga wa India".


"Baadhi ya watu wameufanya mchezo wa kisiasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita," aliongeza.

Chanzo- BBC Swahili

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments