MISA TANZANIA YAWANOA WAANDISHI IRINGA JUU YA SHERIA ZINAZOSIMAMIA TASNIA YA HABARI


TAASISI ya vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara (Media Institute of Southern Africa - MISA Tanzania) imekutanisha waandishi wa habari na  wadau  wa  habari  mkoa  wa  Iringa kwa  lengo la kuwajengea uwezo  kuhusu sheria mbalimbali za habari za vyombo vya habari nchini Tanzania.


Akizungumza  wakati wa mafunzo hayo  yaliyofanyika  jana katika  Hoteli ya  Gentle Hill mjini  Iringa Kaimu mkurugenzi wa MISA Tanzania Andrew Marawiti  alisema mafunzo hayo ni  mwendelezo wa mafunzo ambayo MISA Tanzania imeendelea  kutoa kwa  wana habari wa  mikoa  mbali mbali nchini lengo ni  kuwajengea  uwezo  wa  kutambua na kuchambua sheria  hizo  pamoja na kutoa maoni yao.

Alisema kuna changamoto ya mwitikio kutoka kwa waandishi  kujitokeza  ipasavyo katika kupaza sauti kujitetea wenyewe  juu ya  sheria  hizo  ili pale inapowezekana  ziweze  kufanyiwa marekebisho  ili  zisiwe  mwiba kwa  wahabari na  vyombo  vya habari .

“Maslahi ya mwana habari yatatetewa na mwandishi mwenyewe hivyo waandishi ni jukumu letu kujitambua na kupaza sauti juu ya matatizo na changamoto zinazo tukumba katika utendaji kazi wetu nia ni kuifanya tasnia ya habari ikue na iheshimike”,alisema.

Alisema  kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi hao ili kutambua maudhui ya sheria hizo.

“Tunachofanya kupitia mafunzo haya ni kuwaonesha na kuwasaidia Waandishi  wa Habari wapate uelewa wa sheria ambazo zinasimamia tasnia yao”,aliongeza

Alisema kuwa  kupitia mafunzo hayo waandishi watakuwa na uwezo wa kushiriki mijadala mbalimbali ikiwemo ile ya mabadiliko ya baadhi yaa vifungu katika sheria hizo ambazo zinaonekana kuminya uhuru wa kujieleza.

Mwezeshaji  wa  mafunzo hayo  mwanahabari  mkongwe Jesse Kwayu  alisema kwenye  sheria   hizo kuna mambo mengi mazuri  lakini mazuri hayo yanafunikwa na vifungu vichache vinavyominya uhuru wa habari na kujieleza.

Kwayu  aliwataka  waandishi wa habari kuzisoma sheria hizo na kuzielewa ili wawe na uelewa juu ya vifungu mbalimbali katika sheria hizo.

“Sheria tulizonazo ukizisoma kwa wepesi utaziona ni nyepesi lakini ni sheria nzito sana,na Mwandishi ili akamilike lazima azifahamu sheria hizi ..sheria hizi zipo nyingi ila kutokana  na utendaji kazi tutajikita katika sheria tatu ambazo sheria ya vyombo vya kielektroniki “EPOCA”, sheria ya takwimu “STATISTICS ACT” na sheria ya vyombo vya habari “MEDIA SERVICE ACT 2016”,alisema Jesse Kwayu.

Alisema sheria hizi zimekuwa zikilaumiwa kuwa zinakinzana na uhuru wa habari kwa mwandishi wa habari hivyo lengo kubwa ni kutoa uelewa waandishi wa zijue sheria hizo na ipaze sauti ili ziweze kufanyiwa marekebishpo kwa ustawi wa tasnia ya habari

Kwa  upande  wake mdau  wa habari  kutoka  Asasi ya  kiraia ya  ICISO  mkoani  Iringa Raphael Mtitu  aliwataka  waandishi wa Habari kushirikisha taasisi za  kiraia  katika mapambano ya kudai haki kujieleza kwa vile ni matakwa ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Alisema  haki hiyo inamgusa kila mwananchi hivyo ni vyema taasisi zote zikaungana kupigania haki hiyo.

“Msione hili jambo ni kwenu peke yenu,kama hivi MISA TAN walivyotushirikisha basi iwe fursa kwa taasisi nyingine za habari kuona umuhimu wa kushirikisha taasisi za kiraia ili kuunganisha nguvu na kuwa sauti ya pamoja” ,alisema Mtitu. 

"Tuungane pamoja katika harakati za kudai uhuru wa habari,linapomtokea mwenzako leo kesho linaweza kuwa kwako.Mmoja wetu akipatwa na tatizo tusiiache MISA Tanzania pekee",aliongeza.

Kwa upande wao  baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo,wamewataka waandishi wa habari wote kuungana pamoja katika kutetea maslahi ya tasnia.

Denis Nyali  ambaye ni mmoja kati ya  walioshiriki warsha  hiyo alisema kuna mambo mengi yanayosonga utendaji wa wanahabari nchini lakini kwa mara kadhaa waandishi hawatoi ushirikino katika kutatua changamoto za wenzao.

 Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari Iringa (IPC) Frank Leonard akichangia maoni yake alisema miongoni mwa sheria zinazokiuka uhuru wa waandishi ni sheria inayowataka waandishi kuanza kutambulika kuanzia ngazi ya Stashahada ya Habari na kuendelea 

“Kuna waandishi wa habari wana Shahada moja wengine mbili lakini ukiwaambia waandike story (habari) hata paragraph moja hawawezi huu ni mtihani lakini wapo ambao wana cheti tu na wana uwezo wa kuandika stori nzuri kabisa ambayo ni zaidi hata ya huyu mwenye elimu kubwa amesema” alisema Leonard.

Huku  washiriki  wa mjadala   huo  wakitamani sheria  ipitishwe kwa mtu  kuwa mbunge lazima  awe na kiwango  cha  elimu kuanzia Diploma  kama  wanahabari  ili  awe na utashi mkubwa wa kuchambua na kutunga sheria  mbalimbali  za nchi .

"Wabunge  wanapitisha sheria  ya  kikomo  cha  elimu kwa wanahabari  kuwa ni Diploma  wakati   ili  mtu  uwe  mbunge kigezo  kikubwa ni kujua  kusoma  na kuandika  na kuwa ingependeza na  wao  wabunge kigezo cha elimu  kitiliwe mkazo",walisema

Naye mwanahabari  Ibrahim Kitang’ala alisema  kuwa sheria hizi nyingi zinapitishwa na wabunge ambao kigezo chao cha kuwa mbunge ni walau awe na elimu ya darasa la saba tu. 

“Unakuta mbunge ana elimu ya darasa la saba halafu anapitisha sheria mwaandishi  wa habari niwe na Stashahada  huyu wa darasa la saba anajuaje stashahada”, alisema Kitang’ala.

"Kuwa  wabunge  wanapitisha sheria  ya  kikomo  cha  elimu kwa wanahabari  kuwa ni Diploma  wakati   ili  mtu  uwe  mbunge kigezo  kikubwa ni kujua  kusoma  na kuandika  na kuwa ingependeza na  wao  wabunge kigezo cha elimu  kitiliwe mkazo",aliongeza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments