MGEJA AMPA TANO RAIS SAMIA KUKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA


NA BALTAZAR MASHAKA,Kahama

MWENYEKITI wa Tanzania Mzalendo Foundation , Khamis Mgeja, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali na kukutana na viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa siasa nchini.
 
Amesema uzuri zaidi  na muhimu ni hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano huo kusheheni  mambo mazito yenye manufaa na maslahi mapana  ya nchi hususani ustawi wa demokrasia na maendeleo.

Mgeja alitoa kauli hiyo leo ofisini kwake mjini Kahama,Mkoa wa Shinyanga,alipozungumza na waandishi wa habari waliotaka kupata maoni yake kuhusu Rais Samia,  kukutana na viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa siasa pamoja na hotuba aliyoitoa.

Alisema kitendo alichokifanya Mh. Rais Samia cha kukutana na viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa siasa kinapaswa kupongezwa na kila raia mwema mwenye mapenzi ya kulitakia heri taifa letu,kina kwenda kufungua ukurasa mpya wenye mwanga, nuru na matumaini yenye ustawi wa demokrasia nchini.
"Nawaomba sana kwa heshima na kuwaasa viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa siasa kuitafsiri hotuba ya Rais Samia kwa vitendo vya kweli ya dhati,"alisema Mwenyekiti huyo wa taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation inayojihusisha na haki,demokrasia na utawala bora.

Mkongwe huyo wa siasa nchini alisema kila mpenda demokrasia lazima afurahie Rais Samia kukubali kukutana   na wanasiasa hao, ni ukweli usiopingika ameonyesha dhamira ya kweli na nia yake njema ya kuwaunganisha Watanzania kuwa wamoja,wenye upendo na mshikamano kama taifa, hatimaye kujiletea maendeleo ya haraka kwa manufaa ya wananchi wote bila kujali dini,kabila,rangi itikadi na ubaguzi wa kijinsia.

Mgeja aliwashauri wanasiasa na vyama vyao watumie fursa hiyo adhimu ya kukutana na Rais Samia,wafanyie kazi waliyoyasikia kupitia hotuba yake hiyo,pia  aliwaomba wakubali kubadilika  hasa baadhi ya viongozi waviondoe vyama vyao kwenye uanaharakati na kuvifanya vya kisiasa vitakavyozingatia sheria, kanuni na misingi halisi ya shughuli za siasa za kistaarabu.

" Demokrasia ni jambo zuri linapoendeshwa kwa ustaarabu kwa ustawi  wa wananachi, demokrasia ikitumiwa vizuri na kila mmoja wetu hata pakitokea ushindani wa kisiasa wa vyama vya siasa hushindana kwa hoja na majibu pia hupatikana kwa hoja," 

"Bahati mbaya baadhi ya vyama na wanasiasa wamekuwa hawaitendei haki demokrasia, wanashindwa kuwalisha wananchi matunda mazuri ya demokrasia hiyo," alieleza Mgeja na kuvitahadharisha kuwa ikitokea fursa ya kufanyika mikutano ya hadhara wananchi hawatarajii tena kurudishwa walikotoka na wanasiasa pamoja na vyama vyao.

Alieleza zaidi wasisimame kwenye majukwaa na kutoa maneno ya kejeli na wakifanya hivyo bila kuwa na hoja watakuwa hawatoshi na itadhihirika kuwa wanasiasa hao wamefilisika  kisiasa.

Mwenyekiti huyo wa zamani wa CCM Mkoa wa Shinyanga, alisema wingi wa vyama vya siasa si hoja, hoja ya msingi ni je, wana sera mbadala wa chama kilichopo madarakani zinazogusa maisha ya wananchi, na hivyo ni vema wanasiasa wa aina hiyo wajitathmini upya.
Aliwaomba na kuwasistiza wanasiasa na vyama vyao kuitendea haki demokrasia wakizingatia nasaha za Rais Samia aliposistiza umuhimu wa utii wa sheria huku akimnukuu ; 
"Wanasiasa na Watanzaniakama kuna tofauti zetu tuzizike, tufungue ukurasa mpya na maelewano ndani ya Tanzania, tuonyeshane upendo na mshikamano kwa kufuata mila,desturi na sirika ya Kitanzania na muktadha wa hali ya kiuchumi ya nchi yetu."

Alinukuu zaidi akisema sisi ni taifa moja , hakuna mwenye hati milki ya Tanzania, sote ni Watanzania  tuna haki sawa mbele ya sheria na mbora wetu ni yule anayezingatia na kufuata sheria , hivyo maneno hayo aliyoyasema Rais Samia ni muhimu kuyazingatia, ni nyeti na yana tija kubwa kubwa kwa taifa.

Mgeja pia aliishauri serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, hotuba hiyo ya Rais Samia kutokana na kusheheni mambo muhimu kwa ustawi wa taifa na mustakabali wake, kwa heshima ikiwapendeza kwa faida ya uelewa kwa kila Mtanzania.

Aliomba hotuba hiyo ichapwe kwenye jarida maalum  na kusambazwa hadi vijijini kwa wananchi na kizazi cha sasa hata wasio wana siasa kwa unyeti wake na mustakabali wa misingi ya demokrasia na maendeleo waisome.sssss 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments