KAMISHNA WA ARDHI AWATAKA WATANZANIA KULIPA KODI YA ARDHI

 

Kamishna wa Ardhi , Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Nathaniel Nhonge 

Dotto Kwilasa Malunde 1 blog, Dodoma

KAMISHNA wa Ardhi , Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Nathaniel Nhonge  amewataka  watanzania  kulipa kodi ya pango la ardhi kabla ya Januari Mosi mwakani  ili  kuepuka riba ya asilimia moja ambayo watatozwa kila mwezi kama faini endapo  watachelewa kulipa kodi hiyo.


Hayo yameelezwa leo Alhamis  Desemba 30,2021 Jijini Dodoma  na Kamishna huyo wakati alipokuwa   akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kodi ya  pango hilo la Ardhi ambapo amesisitiza kuwa ulipaji wa kodi ni maendeleo .


Kamishna Nhonge amesema watanzania wengi wameitikia wito wa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa mwaka huu  hivyo amewataka kuendelea kulipa kwani ifikapo Januari mosi mwakani watatakiwa kulipa faini ya  riba ya asilimia moja kwa mwezi.

“Kwa maana ikifika tarehe moja  mwezi wa kwanza kwa maana ile kodi yako inaanza na riba sisi msisitizo wetu ni kilipa kipindi hichi cha miezi sita ambayo haina riba sasa kila mwezi sasa inaanza kuongezeka tunaona ni muhimu kuwaambia wananchi muda upo baada ya tarehe 31 tutaanza kutoza na riba,”amesema.

Aidha Nhonge amesema Wizara hiyo imeweka utaratibu mzuri  ili kuhakikisha wanatoa huduma bora za ulipaji kodi ambapo wameanzisha kituo cha mawasiliano kwa wateja na  wanaweza kuwahudumia wananchi popote walipo ili kuwawezesha kulipa kodi.

Vilevile amesema  mikakati ya Wizara hiyo  ni kuhakikisha ina pima ardhi kwa kasi ili kila Mtanzania aweze kumiliki ardhi ambapo tayari Wizara hiyo ilishapokea fedha kiasi  cha Shilingi bilioni 50 kutoka Serikalini kwa ajili ya kazi hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha kodi Wizara ya Ardhi,Nyumba na maendeleo ya Makazi Denis Masami amesema kuwa katika kipindi cha kuelekea mwisho wa mwezi mwitikio  wa ulipaji kodi ya pango la ardhi umeongezeka na wengi wamejitokeza kulipa.

Amesema  hadi sasa wameshakusanya kiasi cha Shilingi bilioni 60 na malengo ni kukusanya bilioni 221.

“Sasa hivi ukusanyaji umeongezeka kwa wiki tunakusanya  bilioni 2 mpaka 4  kwa Jiji la Dodoma kwa mwaka huu  kulikuwa na  wamiliki 250 waliokuwa  wanalipa lakini  sasa hivi  wamiliki ni  890  kwa wiki hata kiwango tulichokuwa  tunakusanya kilikuwa  milioni 60 mpaka 70 sasa hivi mpaka milioni 200",amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post