WAKANDARASI SINGIDA WAKABIDHIWA ZAIDI YA BILIONI 12 KUKAMILISHA MIRADI YA BARABARA VIJIJINI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kulia) akikata utepe kuzindua hafla fupi ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi na matengenezo ya Barabara kati ya Wakandarasi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani singida leo Tarehe 1 Desemba 2021. Wengine katikati ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Juma Kilimba na Mratibu wa Tarura Mkoa wa Singida, Mhandisi Tembo Davascar
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge (kulia) akionesha Mkataba baada ya kuzindua hafla fupi ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi na matengenezo ya Barabara kati ya Wakandarasi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani singida leo Tarehe 1 Desemba 2021. Wengine katikati ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Juma Kilimba na Mratibu wa Tarura Mkoa wa Singida, Mhandisi Tembo Davascar
Zoezi la Utiaji saini wa mikataba hiyo likiendelea
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza kwenye hafla hiyo
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Juma Kilimba akizungumza kwenye hafla hiyo
Mratibu wa Tarura Mkoa wa Singida, Mhandisi Tembo Davascar akitoa taarifa fupi ya mwenendo mzima wa zoezi hilo
Wahandisi mbalimbali wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.
Wahandisi mbalimbali wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.

Na Edna Malekela, Singida
JUMLA ya mikataba 26 ya matengenezo ya barabara za Vijijini na Mjini yenye thamani ya shilingi bilioni 12.6 imesainiwa kati ya Wakandarasi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini mkoani hapa (TARURA) huku Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge akishuhudia zoezi hilo.

Akizungumza leo wakati wa hafla hiyo, Mratibu wa Tarura mkoa wa Singida, Mhandisi Tembo Davascar, alisema mikataba hiyo 26 ya awamu ya pili itahusisha matengenezo na ujenzi wa barabara zilizopo wilaya za Ikungi, Manyoni, Mkalama, Itigi, Iramba na Singida Vijijni.


Hata hivyo, Davascar alisema wametoa siku 14 kuanzia sasa kwa wazabuni hao kujipanga na kuandaa vikosi kazi vyao na baada ya hapo watatakiwa kutekeleza mikataba yao ndani ya kipindi kisichozidi miezi 6 baada ya siku hizo

“Ratiba ya utekelezaji wa hii mikataba itaanza siku 14 kuanzia sasa, na kuanzia Desemba 15 wanapaswa kuanza mara moja utekelezaji wa mkataba kwa kipindi kisichopungua miezi 6,” alisema Mratibu huyo wa Tarura Mkoa.

Awali akizungumza kabla ya zoezi la utiaji saini, Dkt Mahenge aliwahimiza na kuwakumbusha wakandarasi kuzingatia kikamilifu ratiba ya utekelezaji wa mikataba hiyo bila ya kuingiza visingizio vyovyote vinavyoweza kukwamisha ustawi wa miradi hiyo muhimu kwa maendeleo


Aidha, alisisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia ubora na viwango sambamba na kutanguliza uzalendo wakati wa utekelezaji wake kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa ambazo ni chimbuko la kodi za wananchi katika muktadha chanya wa matumizi endelevu kwa vizazi vya sasa na baadaye.


“Nikiwatazama wahandisi wote hapa mnaosaini mikataba ya ujenzi wa barabara hizi ni wazawa, sitarajii kuona virusi vyovyote vinajitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hii ambayo Mheshimiwa Rais ameamua bilioni hizi 12.6 zielekezwe kwetu kwa ajili ya barabara za vijijini pekee…naomba tusimwangushe, na tusiwaangushe walipa kodi waliowezesha hili kufanyika,” alisema Dkt. Mahenge


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba, akiwa miongoni mwa walioshuhudia zoezi la utiaji saini alipongeza serikali kupitia chama hicho kwa kutekeleza yale yalioelekezwa kwenye ilani


“Hakikisheni fedha zilizotolewa zinakwenda kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa…nawasihi sana wakandarasi msiende kuboronga, mana kama mtaharibu ahadi hizi ambazo chama na serikali tuliahidi kwa wananchi mjue mwisho wa siku atakayelaumiwa na kupigwa mawe ni sisi chama na sio ninyi,” alisema Kilimba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments