MKURUGENZI WA MANISPAA ATOA UFAFANUZI TOZO ZA TAKA ZILIZOZUA MJADALA SHINYANGA MJINI , ASEMA "SIYO TOZO MPYA, NI JUKUMU LA JAMII KUZOA TAKA"

Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021 kuhusu ada za uzoaji wa taka ngumu katika Manispaa ya Shinyanga. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021 kuhusu ada za uzoaji wa taka ngumu katika Manispaa ya Shinyanga.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura ametoa ufafanuzi kuhusu mjadala unaoendelea kuhusu ada za uzoaji wa taka ngumu akisema tozo hizo ambazo zinalalamikiwa na wananchi kuwa ziko juu kuwa siyo tozo mpya bali zipo kwa mujibu wa sheria ndogo ya Manispaa ya Shinyanga iliyopitishwa mwaka 2014 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2019.


Akizungumza na Waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021, Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Shinyanga amesema ada hizo za uzoaji taka zilizoanza kutozwa kwa wananchi Desemba 1,2021 kupitia kwa kampuni ya Ukandarasi ya Networking Youth Group ya Jijini Arusha siyo tozo mpya.

“Kumekuwa na mijadala kuhusu tozo za uzoaji taka ngumu katika Manispaa ya Shinyanga. Napenda kuwaeleza wananchi kuwa hizi tozo zinazotozwa sasa hivi siyo tozo mpya bali zinatokana na Sheria ndogo ya Manispaa ya Shinyanga ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 ambayo ilizingatia hatua zote muhimu ikiwemo kujadiliwa na wananchi, Baraza la Madiwani na kupitishwa na Waziri mwenye dhamana”,amesema Satura.

“Kwanini mabadiliko haya yanaonekana sasa badala ya kutumika tangu sheria ilipotungwa?,Kwanza naomba niweke wazi kuwa jukumu la kuzoa taka ngumu ni wajibu wa mwananchi na wajibu wa kuteketeza taka ni jukumu la Serikali. Siku za nyuma Halmashauri haikumtwisha mwananchi mzigo wa kuzoa taka hivyo shughuli za uzoaji taka na kuzipeleka kwenye dampo zilikuwa zinafanywa na Halmashauri kupitia vikundi vya kijamii. Halmashauri ilikuwa inatumia takribani shilingi Milioni 30 kila mwezi kwa ajili ya uzoaji taka, jukumu ambalo siyo lake, hivyo tulikuwa tunaisaidia jamii”,amesema Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga.

“Siyo wajibu wa Halmashauri ya Manispaa kuchukua taka kutoka kwenye maghuba na kupeleka kwenye dampo.Tulikuwa tunabeba jukumu hilo,tumeona hizo gharama ni bora zirudi kwa wananchi wenyewe. Sisi tumejiondoa kwenye uzoaji taka kutoka kwenye maghuba kwenda kwenye dampo. Wajibu wa jamii ni kukusanya taka na kuzipeleka kwenye dampo na sisi wajibu wetu kama Serikali ni kuteketeza taka ngumu kwa kuzingatia aina za taka”,amefafanua Satura.

Amesema Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imekabidhi Sheria ndogo iliyopitishwa mwaka 2014 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2019 kwa Kampuni ya Networking Youth Group ya Jijini Arusha ambayo inakusanya taka kwa kutumia magari katika kata tano za kimkakati ambazo ni Kambarage, Mjini, Ngokolo, Ibinzamata na Ndembezi na kwenye kata zingine vikundi vya kijamii vitaendelea kukusanya taka ngumu.

“Huyu Mkandarasi anayekusanya taka tumempatia sheria hizi na hizi tozo siyo mpya. Sheria inasema hivyo hakuna aliyezipanga hivyo wananchi waendelee kulipia tozo hizi ili kuhakikisha tunaondoa taka katika Manispaa yetu ambayo tunataka iwe Jiji”,amesema.


Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kuwataka Viongozi wa serikali za mitaa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ada za uzoaji taka ngumu kwenye maeneo yao ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Zoezi la uzoaji wa taka ngumu likiendelea katika ghuba la Soko Kuu Mjini Shinyanga
Ufafanuzi huo wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga unatokana na malalamiko ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga  ambao wanasema Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imepandisha ghafla ada za uzoaji wa taka ngumu kuanzia Desemba 1,2021 kwa mujibu wa sheria ndogo za Manispaa ya Shinyanga .

Katika malalamiko hayo mfano wamesema mtu aliyekuwa analipa shilingi 2,000/= sasa atalipia shilingi 5000/= na upande wa taasisi zilizokuwa zinalipa shilingi 3000/= sasa watalipa shilingi 10,000/= huku aliyekuwa analipia shilingi 10,000/= sasa atatakiwa kulipa shilingi 50,000/= kwa mwezi.

Kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wanasema licha ya kwamba jambo la ada za taka ni la lazima lakini ada hizo mpya ni kubwa kuliko gharama za awali hivyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kupunguza ada hizo.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments