MANISPAA YA SINGIDA YAKUTANA NA WATENDAJI WAKE WA KATA KUTATUA CHANGAMOTO


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu  akizungumza na maafisa watendaji wa kata
Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Zefrin Lubuva akizungumza na maafisa watendaji wa kata
Kikao kinaendelea
Kikao kinaendelea

**
Na Edina Malekela ,Singida

Halmashauri ya Manispaa ya Singida imeanza utaratibu wa kukaa na Watendaji wa Kata ndani ya Manispaa hiyo ili kubaini na kutatua changamoto wanazokumbana nazo.

Utaratibu huo uliibuliwa baada ya kikao kazi cha Watendaji Mstahiki Meya na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo  Yagi Kiaratu kilichoketi juzi katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo.


Awali akifungua kikao hicho jana Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Yagi Kiaratu alisema kuwa Halmashauri imeamua kuanza kuwaangalia watendaji wake kwa kuwapa shajala pamoja na pesa tasilimu shilingi laki tano kwa kila kata ili kusaidia shughuli za kiutawala.


"Tunafanya haya yote kwenu ili nanyi mfanye kazi nzuri ya kukusanya mapato na katika hili Halmashauri yetu hatuna utani tuwe tunakufahamu ,uwe mtoto wa Mjomba au uwe mchapa kazi katika maeneo mengine lakini kama utafeli katika swala la kukusanya mapato kwa kweli hatutakuvumilia", alisema.

"Mtendaji wakata au wakijiji moja ya kipimo cha utendaji ni ukusanyaji wa mapato Halmashauri yenye mapato mazuri inaweza kutoa huduma nzuri kwa wananchi wake nendeni mkafanye kazi sasa hivi nguvu mnayo", alisema Kiaratu"

Alisema lengo la Halmashauri ya Manispaa ya Singida ni kutoa huduma nzuri kwa wananchi wake huku akiwataka watendaji kuangalia ripoti ya miaka ya nyuma ambapo Halmashauri ilikuwa ikisomeka kuwa ya mwisho lakini sasa imepiga hatua ambapo kati ya Halmashauri 20 za Manispaa hapa nchini Manispaa ya Singida imekuwa ya 4 katika ukusanyaji wa mapato.

"Tumewaita kuongea na nyinyi leo hapa baada ya kuona mmeshaongea na Maafisa utumishi mara nyingi lakini hatuoni mabadiliko kuna kata kila taarifa ikija zinashida sasa mmepata nguvu jamani mkafanye kazi" ,alisema Kiaratu.


Aidha alizitaja kata ambazo zinasuasua katika ukusanyaji wa mapato kuwa ni kata ya Unyanga,Uhamaka na Kisaki,Licha ya kuwa na vyanzo mbalimbali vya mapato,hivyo akazitaka kuhakikisha zinasimamia ipasavyo vyanzo hivyo ili kuongeza kiwango cha mapato.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Zefrin Lubuva aliwataka Watendaji hao kwenda kusimamia vyema vyanzo vya mapato ili kuiweka Halmashauri hiyo katika nafasi nzuri kitaifa


"Hapo mbeleni mimi Mkurugenzi ,Mstahiki Meya na viongozi wengine tutapita huko kushiriki na kuona maagizo yanavyotekelezwa hasa maagizo ya kitaifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa tutapita kuona", alisema Lubuva.


Aidha aliwataka watendaji kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine ili kufikia lengo la Halmashauri katika kukusanya mapato hali itakayosaidia kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.


Naye Mwenyekiti wa Watendaji Futalishauri Mwandi aliishukuru Halmashauri kwa niaba ya Watendaji kwa kuona umuhimu wa Watendaji na kuwapa vitendea kazi.

Alisema kuwa tangu Mwaka 2016 Watendaji hawakuwahi kupewa vitendea kazi hali iliyowalazimu kutumia fedha zao ili kuhudumia wananchi wao.

"Tunamshukuru Mkurugenzi wetu ndugu Zefrin Lubuva kwa kutuona na kuona umuhimu wetu, sisi watendaji tunamshukuru sana na tunaenda kufanya kazi kwa kushirikiana na watendaji wa mitaa", alisema Futalishauri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments