WAZIRI PROF. MKENDA : SEKTA YA KILIMO INACHANGIA 26% YA PATO LA TAIFA NA KUTOA AJIRA KWA 58% - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Sunday, November 28, 2021

WAZIRI PROF. MKENDA : SEKTA YA KILIMO INACHANGIA 26% YA PATO LA TAIFA NA KUTOA AJIRA KWA 58%

 Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog, DODOMA.


SEKTA ya kilimo imeajiri asilimia 58 ya Watanzania ikilinganishwa na asilimia 90 wakati wa uhuru, hali inayoashiria kukuza uchumia na kuongeza pato la Taifa.


Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na  Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya wizara yake kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru.


Amesema mchango wa sekta ya kilimo kwenye pato la Taifa umekua kutokana na  hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini na kusaidia kuongeza  pato la Taifa kwa  asilimia 26.


Licha ya hayo ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua katika kuimarisha uzalishaji wa alizeti na chikichi hapa nchini ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa kupunguza uagizaji toka nje.


"Katika kipindi cha miaka 60, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya kilimo hapa nchini,matokeo ya hatua hizo ni Taifa kujitosheleza kwa chakula na kuzalisha ziada inayouzwa nje ya nchi,"amesema. 


Akizungumzia mikakati ya Serikali kwa sasa Katika kuongeza tija kwenye kilimo,Prof.Mkenda ameeleza kuwa imejikita katika kuimarisha tafiti, huduma za ugani, kuongeza upatikanaji wa mbegu bora, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na masoko. 


Ameeleza kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa mbolea hapa nchini unakuwa wa uhakika kwa kuvutia wawekezaji kuja kujenga Viwanda ikiwemo kile kinachojengwa hapa Dodoma kitakachozalisha tani laki sita kwa mwaka.


"Kupitia mikakati hii tani milioni 18 za mazao zitazalishwa na ziada ni tani milioni 3,ni hatua nzuri kwani wakati wa kupata uhuru tulikuwa tunazalisha tani 1 ya mpunga kwenye ekari 1 na sasa tani 2.3 hadi 4 kutokana na maboresho kwenye sekta ya kilimo,"amesema Waziri huyo.


Sambamba na hayo amezungumzia utoshelevu wa chakula nchini kuwa kwa sasa ni asilimia 126  ikilinganishwa na wakati tunapata uhuru ambapo Tanzania ilikuwa inaomba msaada wa chakula kutoka mataifa tajiri.


"Mwanzoni kabisa tulikuw√† tunaomba chakula mataifa tajiri kama Marekani lakini Sasa hilo halipo tunajitegemea wenyewe na sisi kama Serikali tunaweka msukumo zaidi katika kuimarisha ushirika hapa nchini ili kuwasaidia wakulima kupata manufaa zaidi kiuchumi,"amesema. 


Kadhalika Waziri Mkenda amesema huduma za ugani zimeimarishwa zaidi katika kipindi hiki na tayari Serikali inaendelea kuwapatia vitendea kazi ikiwemo pikipiki 2000 ambazo zitatolewa Januari, 2022 na kwamba  86 tayari zimeshatolewa.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

No comments:

Post a Comment

Pages