GGML YATOA BILIONI 9.2 KUTEKELEZA MPANGO WA UWAJIBIKA KWA JAMII


Mkurugenzi wa GGML, Richard Jordinson akisaini mkataba huo wa makubaliano

Na Mwandishi Wetu - Geita
Kampuni ya Anglogold Ashanti – Geita Gold Mining Limited (GGML) na Halmashauri ya Mji Geita na halmashauri ya Wilaya ya Geita, zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) wenye thamani ya TZS bilioni 9.2 kutekeleza Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) katika kipindi cha mwaka 2021/2022.

Kwa kutia saini makubaliano hayo, GGML inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya dhati kwa serikali ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla kwamba inafuata kikamilifu misingi na taratibu zilizopo katika Kifungu cha 105 cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho 2017.

Kifungu hicho kinazitaka kampuni zilizowekeza kwenye sekta ya madini nchini kutekeleza mpango huo wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii.

Utekelezaji wa mpango huo wa CSR utanufaisha jamii za Geita katika maeneo mbalimbali kama mazingira, miundombinu, afya, elimu na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs).

Katika hafla fupi ya kutia saini makubaliano hayo juzi mjini Geita, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule ameipongeza kampuni hiyo kutokana na ushirikiano imara uliopo kati yake na Serikali tangu kuanzishwa kwake.

“GGML imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa mpango huu wa Uwajibika wa Kampuni kwa jamii (CSR), na makampuni mengine yamekuwa yakija kujifunza kutoka hapa na hata kuwa mfano katika machapisho mbalimbali ya kitafiti kutoka vyuo vikuu nchini.

“Watanzania wanaofanya kazi katika makampuni mengine wanatakiwa kuendelea kutuwakilisha vizuri katika makampuni hayo kama ilivyo kwa GGML. Wanatakiwa kufanya kazi kwa uadilifu,” alisema.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Richard Jordinson alisema GGML inajitahidi kuunga mkono Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo endelevu kijamii na kiuchumi. Kampuni pia inafanya kazi na serikali za wilaya na jamii inayozunguka mgodi kwa kusimamia na kutekeleza miradi muhimu kwa mustakabali endelevu wa mkoa wa Geita.

"Tunafuraha kwamba dhamira yetu kwa Serikali ya Tanzania na jamii ya Geita inaendelea kutekeleza. Sasa katika mpango wetu wa nne wa CSR tangu marekebisho ya Sheria ya Madini yafanyike, tuna matumaini tunaweza kuendeleza miradi ya awali tuliyokuwa tumeahidi kuitekeleza ndani ya jamii. Lengo ni kuendelea kushirikiana katika miradi endelevu inayoweza kustahimili maisha ya mgodi,” alisema.

Alisema GGML imeshirikiana kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa na sekta binafsi kusaidia miradi kadhaa katika mkoa wa Geita ukiwemo mradi wa maji ya bomba katika Mji wa Geita uliosaidia kuongeza idadi ya wananchi wanaopata maji safi na salama kutoka asilimia tatu hadi asilimia 40 kati ya 2016 na 2020.

Alisema GGML pia inaendesha programu ya kampeni mbalimbali katika ngazi ya kitaifa, ikiwamo GGML Kili Challenge ambayo inalenga kuendeleza mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

“Kampeni hiyo imechangia zaidi ya Sh bilioni 1.3 katika miradi ya kuzuia VVU na kuwezesha matibabu kwa waathiriwa nchini kote tangu 2018.

“Pia GGML imetekeleza miradi mbalimbali katika jamii ya Wana-Geita, ikiwemo huduma ya maji, elimu na maendeleo ya kiuchumi katika sekta ya kilimo, usafiri na huduma nyingine ambazo ziligharimu zaidi ya Sh bilioni 50 tangu GGML ilipoanza kazi zake hapa nchini mwaka 2000,” alisema.

Alisema Kampuni hiyo imetumia dola za Marekani bilioni 1.7 (Sh trilioni 3.9) kulipa kodi kwa serikali tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000.

Aidha, mbali na CSR na kodi, kampuni hiyo pia imetengeneza mazingia ya kibiashara kwa kampuni za ndani kufanya biashara na GGML yenye thamani zaidi ya Sh bilioni 67.6 zilizotumika katika ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali za hadi kufikia mwishoni mwa Septemba 2021.

“GGML imeshirikiana na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kuwaongezea ujuzi wafanyabiashara zaidi ya 350 wa Geita kwa kuwapatia mafunzo ya namna ya kupata zabuni katika miradi mbalimbali.

“Haya yote yameiwezesha kampuni hii kutajwa kuwa kampuni iliyofanya vizuri zaidi katika sekta ya madini Tanzania kwa mwaka wa fedha 2019/2020 baada ya kushinda tuzo za uwajibikaji kwa jamii, mazingira na usalama, malipo ya mapato ya serikali (kodi) na mazingira bora ya ufanyaji biashara ndani ya nchi,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akisaini mkataba huo wa makubaliano. Anayemshuhudia ni Makamu Rais wa GGML, Simon Shayo
Mwanasheria wa Kampuni ya GGML, David Nzaligo (kushoto) akisaini mkataba huo wa makubaliano. Kulia ni Mkurugenzi wa GGML, Richard Jordinson
Baadhi ya wageni waalikwa walioshuhudia utiaji saini mkataba huo wa makubaliano
Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo akizungumza katika hafla hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule akizungumza katika hafla hiyo
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo akizungumza katika hafla hiyo


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments