RAIS SAMIA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA WIKI YA USALAMA BARABARANI KITAIFA JIJINI ARUSHA.. RPC MASEJO ATOA UTARATIBU

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani Kitaifa ambayo yatayofanyika kuanzia Novemba 11,2021 hadi Novemba 20,2021 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari leo Jumanne Oktoba 19,2021 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo amesema wanatarajia mgeni rasmi  kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hivyo kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo ili kujifunza na kupata elimu pamoja na kufanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri.

"Natumia fursa hii kuwajulisha kuwa, Baraza la Taifa la Usalama Barabarani limeteuwa mkoa wetu wa Arusha kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa yatakayofanyika kuanzia tarehe 15/11/2021 hadi tarehe 20/11/2021 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo kauli mbiu inasema JALI MAISHA YAKO NA YA WENGINE BARABARANI",amesema Kamanda Masejo. 

"Katika Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama barabarani tutakuwa tukiendelea na utoaji wa Elimu na ukaguzi madhubuti wa vyombo vya moto barabarani katika uwanja wa maonesho wa Sheikh Amri Abeid na maeneo mbalimbali ya mkoa wa Arusha na viunga vyake",ameongeza Kamanda Masejo 

Amesema pia kutakuwa na mabanda ya wadau mbalimbali ya maonesho yatakayoelimisha na kutoa huduma mbalimbali kama vile Banda la Jeshi la Polisi, TIRA, LATRA, RSA, FIRE, AFYA,RED CROSS,ROTARY CLUB,VETA wengine wengi wanaoendelea kujitokeza na kusajiliwa kushiriki maonesho hayo kwenye maadhimisho. 

"Napenda kuwajulisha kuwa siku hiyo tunatarajia viongozi mbalimbali wa kitaifa watahudhuria na tutaendelea kuwafahamisha kadri tutakavyopanga na kamati ya maandalizi. Watu wote mnakaribishwa kuhudhuria na kushiriki kujumuika nasi katika maandalizi hadi kilele cha maadhimisho haya. Niwaombe walio tayari kushiriki nasi katika maonesho hayo kama vile Taasisi za serikali na za binafsi kuwasiliana na katibu mtendaji au mkuu wa usalama barabarani (RTO) wa mkoa wa Arusha",ameeleza Kamanda Masejo.

Kutokana na kwamba jukumu kubwa la Jeshi la polisi ni kulinda Raia na Mali zao, Jeshi la Polisi nchini kupitia kikosi cha usalama barabarani pamoja na Baraza la Taifa la Usalama Barabarani limekuwa na mpango mkakati wa kutekeleza majukumu yake katika maeneo ya Utoaji wa Elimu, kufanya Operesheni na kusimamia sheria za usalama barabarani.

 "Utaratibu huu ni endelevu kwa nchi nzima ambapo ukaguzi wa vyombo vya moto na utoaji Elimu huchagiza Jeshi la Polisi kuadhimisha wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kitaifa ambayo ufanyika kila mwaka katika maeneo tofauti tofauti",ameongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments