RAIS SAMIA AZUIA WANANCHI KUONDOLEWA KATIKA ENEO KINGA HIFADHI YA SERENGETI


Na Munir Shemweta, WANMM SERENGETI
Rais Samia Suluhu Hassan amezuia  wananchi kuondolewa  katika  eneo kinga (Buffer Zone) la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kutafuta suluhu ya mgogoro wa muda mrefu kati ya hifadhi na wakazi wa vijiji 14 vinavyozunguka hifadhi hiyo

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyopo mkoani Mara ilisogeza mipaka ya eneo  lake la kinga         (Buffer Zone) kwa zaidi ya mita mia tano katika maeneo ya vijiji katika mbuga ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa wilaya za Serengeti na Tarime na kuwafanya wakazi wake kuishi kwa hofu na kushindwa kujua hatma yao.

Vijiji vilivyonufaika na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa upande wa wilaya ya Serengeti ni Bisarara,  Bonchugu, Nyamakendo, Nyamburi, Machochwe, Mbalibali na Merenga na wilaya Tarime ni Gibaso, Kegonga, Kenyamosabi, Nyandage, Nyabirongo, Karakatonga na  Masanga.

Uamuzi huo umetangazwa tarehe 15 Oktoba 2021 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kwa niaba ya Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bisarara wilayani Serengeti mkoa wa Mara.

Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta iko katika ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutoa mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

Hata hivyo, wananchi wa vijiji hivyo wametahadharishwa kuwa na subira baada ya maamuzi hayo ya Serikali mpaka hapo timu ya wataalamu itakapokwenda kubainisha mipaka pamoja na na kuwekwa kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji hivyo.

Waziri Lukuvi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta alisema, serikali kupitia hifadhi ya Taifa ya Serengeti  ilichukua eneo la vijiji 14 katika wilaya za Serengeti na Tarime kwa ajili ya Eneo Kinga (Buffer Zone) la hifadhi na Rais Samia ameridhia mamlaka hiyo irudishe nyuma mipaka yake ili ardhi itumiwe na wananchi.

" Mama anawapenda sana na anajua kuna migogoro midogomidogo ya ardhi lakini kwa sasa ametaka mpokee uamuzi huu kama salamu na hataki shida wala wananchi wake wateseke kwa jambo moja kwa muda mrefu" alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi aliwaambia wakazi wa vijiji hivyo kuwa wamepakana na hifadhi ya mbuga za wanyama namba moja duniani hivyo zawadi pekee watakayompatia Rais Samia kwa uamuzi wa kuwabakisha katika vijiji ni kuimarisha ulinzi kwenye eneo la hifadhi ili mbuga iwe salama.

Wananchi wa kijiji cha Bisarara wameupokea uamuzi wa kupatiwa ardhi eneo la hifadhi ya Serengeti kama ukombozi baada ya kuishi kwa hofu na manyanyaso ya muda mrefu.

Zakaria Petro mkazi wa Msalala Serengeti alisema, uamuzi huo utawafanya wananchi wa vijiji hivyo kuishi kwa amani kutokana na kusumbuliwa na mamlaka ya hifadhi kwa kukamatwa na wakati mwingine mifugo  yao kuchukuliwa.

Naye Mniko Constantino mkazi wa Mugumu Serengeti aliahidi kumlipia gharama ya kuchukulia fomu ya kugombea urais  Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa  mwaka 2025 kutokana na hatua mbalimbali anazochukua kwa kipindi kifupi cha uongozi wake ikiwemo kuwapatia ardhi wananchi wanaishi katika vijiji vilivyokuwa maeneo ya hifadhi.

Mbunge wa Jimbo la Serengeti Dkt Amsabi Mrimi alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuwajali wananchi wa vijiii hivyo na kueleza kuwa mtu anayetoa ardhi kwa wananchi anakuwa amewasaidia kwa kuwa ardhi ndiyo kila kitu.

Ameomba serikali kufanya mrejeo wa sheria ya kuhamisha mifugo katika maeneo ya vijiji vilivyopo kando ya hifadhi kwa kueleza kwamba sheria hiyo imeleta madhara makubwa kwa jamii ya wafugaji.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments