JAPAN YAANZISHA USAFIRI WA UMMA KWA KUTUMIA PIKIPIKI ZA KUPAA ANGANI


Kampuni hiyo inalenga kutengeneza pikipiki za aia hiyo 200 zenye uzito wa kilo 300 kila moja hadi kufikia katikati ya 2022.

Kampuni moja ya Kijapani inatarajia kupiga hatua katika sekta ya uchukuzi na kuwashawishi wamiliki wa magari kukacha magari yao na badala yake kuwekeza kwenye pikipiki zinazopaa kwa kuwekeza dola $680,000.

Kampuni ya ALI Technologies iliweka sokoni pikipiki zake zinazoruka za toleo la X-Turismo Limited zilizoanza kuuzwa nchini Japan mapema Jumatano. Ni pikipiki kubwa zinazotajwa kuwa suluhisho la foleni na shughuli za haraka kwenye miji.

Kampuni hiyo yenye makao yake makuu mjini Tokyo imepata usaidizi mkubwa kutoka kwa kampuni kubwa ya kielektroniki ya Mitsubishi ya Japan, pamoja na mchezaji wa mpira wa miguu wa Japan Keisuke Honda.

ALA Technologies inasema kwamba pikipiki hiyo inaweza kuruka kwa dakika 40 kwa kasi ya hadi kilometa 100 kwa saa ikitumia umeme. Kampuni hiyo inalenga kutengeneza pikipiki za aina hiyo 200 zenye uzito wa kilo 300 kila moja hadi kufikia katikati ya 2022.

Kila pikipiki ina injini maalumu inayowezeshwa na betri nne. "Mpaka sasa, uchaguzi ni kuendelea kutumia ardhi (barabara) au kupaa," alisema Daisuke Katano, Mtendaji mkuu wa ALI Technologies. Akaongeza kuwa Kampuni hiyo ina matumiani ya "kutoa njia mpya ya kusonga (kuruka karibu na ardhi)".

Msongamano ni tatizo kubwa kwa wakazi milioni 13.5 wa Tokyo. Mji wenye teknolojia ya juu, ndio eneo la mjini lenye watu wengi zaidi ulimwenguni.

Lakini sheria za sasa zinakataza pikipiki zinazoruka juu ya barabara ambazo zina shughuli nyingi nchini Japan. Ingawa Bw. Katano anatumaini kuwa timu za uokoaji zitatumia pikipiki mpya za kampuni yake kufikia mahali pasipofikika.
Pikipiki hiyo inaweza kuruka kwa dakika 40 kwa kasi ya hadi kilometa 100 kwa saa.

Magari yanayoruka

Ukiacha pikipiki zinazoruka, dunia imeshuhudia pia magari yanayoruka. Ben Gardner, kutoka kampuni ya Pinsent Masons ya Uingereza, aliiambia BBC kwamba magari (ya kuruka) ambayo hapo awali yalionekana kama vitu visivyowezekana sasa yanazidi kudhihirika kila mwaka.

"Mwishowe, kuna wigo kwetu kuona magari yanayoruka yakienea kote Uingereza," alisema.

Pikipiki inayoruka haifai barabarani chini ya sheria ya sasa ya Uingereza. Lakini Gardner alisema kwa kuzingatia teknolojia mpya katika miaka ya hivi karibuni kunaweza kuashiria uwezekano wa mabadiliko (katika sheria).

"Uzoefu wa sasa wa teknolojia zinazoibuka kama vile magari ya kujiendesha, roboti na ndege zisizo na rubani unaonesha kuwa kuna mwongozo wa aina mpya za usafirishaji kutoka uwanja wa hadithi za kisayansi hadi ulimwengu halisi," alisema.

Mabepari wa ubia, mashirika ya ndege na hata Uber, pamoja na kampuni yake kubwa ya Uber Elephant, wanatoa madai kwa sekta ya magari yanayoruka, ambayo wachambuzi wanasema inaweza kuwa na thamani ya dola $1.5 trilioni ifikapo 2040.

CHANZO - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments