BABA AMUUA KIJANA WAKE KWA DEKI AKIDAI KUTUKANWA



Jeshi la polisi Mkoani Manyara linamshikilia Mkazi wa Kijiji cha Bassoutu wilayani Hanang, Elibariki Shaban kwa tuhuma za kumpiga kwa deki usoni, makofi na mateke mtoto wake wa kumzaa Amos Elibariki (25) na kufariki dunia akikimbizwa Hospitali.

Kamanda wa polisi Mkoani hapa Maresone Mwakyoma akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake leo oktoba 28,2021 alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 26 mwaka huu majira ya saa 3:00 za usiku.

Mwakyoma alisema baba alimpiga mtoto wake huyo baada ya kubishana sana bila kutaja kitu walichokuwa wakibishania.

Alisema baba alipohojiwa na polisi sababu za kumpiga mwanae alisema alimpiga kwa kuwa mtoto huyo alimtukana na yeye hasira ilimpanda na kuamua kumuadhibu kwa kutumia deki, mateke na makofi.

Aidha alisema polisi walibaini Amos alipishana na baba yake ndio maana baba alichukia na kuamua kumpa kichapo na baada ya kichapo alianguka chini. Alisema Amos aliaga Dunia wakati wakimkimbiza kuelekea Hospitali ya Hydom ili apatiwe matibabu.

Katika hatua nyingine polisi wanamshikilia Mfanyakazi wa ndani Januari Makomolwa mkazi wa Kijiji cha Endagikok wilayani Mbulu kwa kumbaka mwanafunzi wa darasa la kwanza(7) jina limehifadhiwa.

Akithibitisha tukio hilo kamanda Mwakyoma alisema lilitokea Oktoba 18 mwaka huu. Alisema Makomolwa ambaye anafanya kazi katika familia ya mtoto huyo inadaiwa aliachiwa mtoto huyo na bosi wake ambaye ni mama wa mtoto ndipo aliamua kuanza kumfanyia unyama.

Mwakyoma alisema mama wa mtoto aliporejea nyumbani alimkuta mfanyakazi wake akimbaka mtoto wake. Alikiri matukio ya ubakaji kuwa mengi katika mkoa huo na akawataka wananchi wanapoajiri wafanyakazi wa ndani wahakikishe wanawachunguza kwanza.

“Tusiwaamini wafanyakazi wa ndani kwa kuwa ndugu wa karibu na marafiki wa familia ndio wanabaka watoto,” alisema Mwakyoma. Aliongeza kuwa jamii kumaliza matukio ya ubakaji kienyeji ni chanzo pia cha kuongezeka kwa ubakaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments