CHONGOLO AZIPA RUNGU KAMATI ZA SIASA ZA WILAYA NA MIKOA FEDHA ZA IMF


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amezipa rungu kamati za siasa za wilaya na mikoa nchini, akisema zitawajibika moja kwa moja iwapo maeneo yao utafanyika ubadhirifu katika utekelezaji wa miradi iliyotokana na fedha za mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Akizungumza katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan, mkoani Arusha, Chongolo alisema anafanya hivyo kwa kuwa, CCM ndiyo iliyounda serikali, ina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi.

Alieleza iwapo litatokea hilo, kamati za siasa zitawajibika moja kwa moja kwa kushindwa kusimamia au kuelekeza utekelezaji wa miradi hiyo.

“Ilani hii sisi ndiyo tuliyoiandaa na tukaitoa kwenda kuiombea kura, ilishinda uchaguzi na sasa ndiyo inatekelezwa, nitoe agizo la kiutendaji kwamba kamati zote za siasa ngazi za wilaya na mikoa yote nchini, popote pale fedha zitakapothibitika zimepotea na ninyi mtawajibika.

“Mtawajibika kwa kutosimamia fedha hizo kwenda kule tulikowaeleza wananchi, kwa sababu kwa kutofanya hivyo, tutakuwa tunaikwamisha Ilani yetu wenyewe kutekelezwa kwa kiwango chenye tija,” alisema.

Chongolo alimpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, kwa kutoa mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo katika wizara zake.

Aliziagiza wizara zote kuhakikisha zinatumia mfano huo kutoa mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo.

Akifafanua matumizi ya fedha hizo na Ilani ya uchaguzi ya CCM, Chongolo alisema kupitia ilani hiyo, Chama kiliahidi kumaliza changamoto ya madarasa kwa shule za sekondari mwaka 2025, lakini Rais Samia ametekeleza hilo kwa miezi sita.

Alisema jambo lingine ni ujenzi wa vituo vya afya, ununuzi wa mashine za X-Ray na mambo mengine ambapo, Rais Samia ameyatekeleza kabla ya muda uliopangwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, aliyekuwa mwanashama wa CHADEMA, Ally Bananga alikihama chama hicho na kuhamia CCM, akisema ndiyo iliyomlea, hivyo amerejea kwa wazazi wake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments