WASIOJULIKANA WAVAMIA OFISI YA MTENDAJI WA MTAA DAR..WAMUUA KWA KUMKATA PANGA


Picha haihusiani na habari hapa chini

Na Said Mwishehe, Michuzi TV
Mauaji ya kutisha yametokea eneo la Mbezi Msumi mkoani Dar es Salaam baada ya watu wasiofahamika kudaiwa kuvamia ofisi za Serikali ya Mtaa wa eneo hilo na kisha kumuua Ofisa Mtendaji kwa kumkata na panga.

Tukio hilo la mauaji limetokea leo Oktoba 11, 2021 kati ya saa sita hadi saa saba mchana wa leo na inadaiwa ofisa huyo mtendaji wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Msumi Jijini Dar es salam ameshambuliwa kwa kukatwa na panga shingoni na watu ambao hawafahamiki.

Akizungumza na Michuzi TV pamoja na Michuzi Blog leo Mmoja wa mashuhuda na mwananchi wa eneo hilo(jina limehifadhiwa) amedai wameshangazwa na tukio hilo la mauaji ambalo limefanywa kwa kiongozi huyo.

Alipoulizwa iwapo watu waliofanya tukio wamefahamika, amejibu hawajafahamika kwani baada ya kutekeleza unyama huo walikimbia na haijulikani ni akina nani na wametoka wapi, ingawa anaamini Jeshi la Polisi linajua namna ya kufuatilia tukio hilo na kuupata ukweli.

"Wananchi tumejawa na taharuki baada ya kutokea tukio hili la mauaji , hatuji nini kimesababisha hadi watu hao kufanya unyama huu kwa kiongozi wa Serikali ya Mtaa,tupo hapa tunasubiri kuona nini kinachoendelea,"amesema shuhuda huyo alipokuwa akizungumza na Michuzi TV

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Ramadhan Kingai aliyezungumza na Michuzi TV amethibitisha kupata taarifa hizo za tukio la mauaji na tayari askari polisi tayari wako eneo la tukio."Tumepata taarifa za tukio hilo,tunafuatilia na baadae tutatoa taaria rasmi kwa vyombo vya habari."

Michuzi TV na Michuzi Blog inaendelea kufuatilia tukio hilo kwa karibu ili kuhakikisha umma wa Watanzania unafahamu ukweli wa tukio hilo kupitia Jeshi la Polisi ambalo limeanza kufuatilia.


Chanzo - Michuzi Blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments