Breaking

Post Top Ad

Monday, October 18, 2021

SPIKA JOB NDUGAI MGENI RASMI MAONESHO WIKI YA AZAKI 'CSO' 2021....FCS YAALIKA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI DODOMA


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF) Lulu Ng'wanakilala (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonesho ya wiki ya Azaki yanayojarajiwa kuanza Oktoba 23 hadi 28,2021 Jijini Dodoma, (wa kwanza kushoto) ni Mkurugenzi wa Taasisi ya TANGO Ramadhan Masel, (wa tatu kushoto) ni Anna Henga Mkurugenzi wa kituo cha sheria LHRC, na (wa kwanza kulia) ni Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF) Lulu Ng'wanakilala akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani) wakati wa mkutano wao kuzungumzia Wiki ya Azaki 2021 Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundations For Civil Society (FCS) Francis Kiwanga akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawamo pichani) wakati wa mkutano huo uliofanyika kwenye Ofisi za FCS Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa kituo cha Sheria na Haki za Binaadam (LHRC), Anna Henga akizungumzia tuzo mbalimbali zitakazotolewa na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima Ocktoba 28,2021.


Na Hughes Dugilo, Dar es Salaam.

Katika kuelekea Wiki ya Azaki inayotarajiwa kuanza rasmi Oktoba 23,2021 wadau mbalimbali wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho hayo hususani wakazi wa Jiji la Dodoma na mikoa ya jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari uliofanyika leo kwenye Ofisi za Foundations For Civil Society (FCS) Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility Tanzania (LSF), Lulu Ng'wanakilala amesema kuwa Mgeni rasmi katika Maonesho hayo anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai.

Amesema kuwa Spika Ndugai ni kingozi anayesimamia Mhimili wa Bunge ambao ni muhimili muhimu kati ya mihimili ya nchi yetu na kwamba atapata fursa ya kuona kazi mbalimbali zinazofanywa na Asasi za Kiraia ambapo kauli mbiu ya maonesho hayo mwaka huu ni ''Azaki na Maendeleo"

Mkurugenzi wa Taasisi ya TANGO Ramadhan Masele, amesema katika siku saba za maonesho hayo kutakuwa na matukio mbalimbali yatakayokuwa yanafanyika Jijini humo.

Ameongeza kuwa moja ya mambo ambayo yatafanyika ni utoaji wa msaada wa kisheria kwenye Mabanda mbalimbali lakini pia kutakuwa na utolewaji wa elimu kuhusu chanjo ya Uviko - 19.

Pia Oktoba 24 kutakuwa na mijadala mbalimbali ikiwano kuangalia namna ambavyo wanashirikiana na Serikali na mengine mengi yanayohusu maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha sheria LHRC,Anna Henga  amesema katika maonesho hayo kutakuwa na utoaji wa tuzo mbalimbali ikiwa ni eneo la jinsia, uwajibikaji kwa Jamii, walemavu, na mengineyo ambapo tuzo hizo zitatolewa na Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima Oktoba 28,2021.

Amefafanua kuwa kuna Asasi nyingi ambazo zinafanya kazi vizuri hivyo watatambua mchango wao katika maendeleo ya nchi kupitia wiki hiyo ya Azaki.

Akihitimisha mkutano huo na waandishi wa habari amesema Azaki watashirikiana na Sekta Binafsi kwenye nyanja mbalimbali, na kuwataka wadau na wananchi wote kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga amesema kuwa wao kama Azaki wanatambulika na Serikali na wanapata ushirikiano mkubwa na chini ya rais Samia Hassan Suluhu kuna mwelekeo mzuri.

Amesema Kuwa katika maonesho hayo pia wanatarajia kujadili maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo aliyatoa kwao nahivyo sehemu ya maonesho hayo ni majadiliano.

Kiwanga ameongeza kuwa katika maonesho hayo wamejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanapata faida kupitia wiki hiyo na katika hilo wanatambua umuhimu wa waandishi wa habari na ndio maana wamekuwa nao nyakati zote.

"Lengo letu kubwa nikuona kila kinachofanyika wananchi wanakipata na kinawafikia hivyo kutakuwa na jobo la waandishi kutoka Dar es salaam na wengine watakuwa wa Dodoma",amesema Kiwanga.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages