WAZIRI JAFO ATAKA WANANCHI KUTUNZA MAZINGIRA, KUIFANYA DODOMA KUWA YA KIJANI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akizungumza na wakazi wa Kongwa kuhusu agenda ya mazingira mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani hapo.
Baadhi ya wakazi wa Kongwa wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani) aliyefanya ziara ya siku moja Wilaya hapo leo kuhamasisha utunzaji mazingira.

Na Dotto Kwilasa, Dodoma.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo ametoa rai kwa wakazi wa Kongwa kutoa msukumo wa dhati katika agenda ya mazingira kwa  kupanda miti rafiki kwa mazingira.

Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Wilayani Kongwa Waziri Jafo ametoa rai hiyo leo  na kuwataka kuunga mkono juhudi za Serikali za kuifanya Dodoma kuwa ya Kijani.

"Ndugu zangu Kampeni ya kukijanisha Dodoma ni endelevu, na Kongwa ni sehemu ya Mkoa wa Dodoma, natoa rai kwenu mpande miti kwa wingi, sambamba na kilimo cha Korosho kama zao la kimkakati" Jafo amesisitiza.

Amesema agenda ya mazingira iende sambamba na upandaji wa miti kwa kila kaya walau miti mitatu ikiwemo ya kivuli na matunda ili jamii iweze kunufaika nayo sambamba na hifadhi ya mazingira ikiwa ni pamoja na ulinzi endelevu wa miundombinu kama vile barabara na madaraja.

 "Kongwa ya sasa si sawa na Kongwa ya zamani kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu kama Ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na mkaa,"amesema Jafo.

Pamoja na hayo Waziri Jafo amesema Ofisi yake imezindua Kampeni Kabambe ya Kitaifa ya Uhifadhi na Usafi wa Mazingira kwa lengo la kunusuru taifa na majanga yatokanayo na uharibifu wa mazingira huku akisisitiza  kuwa kila kaya inapaswa kupanda miti walau mitatu ya kivuli pamoja na matunda hali itakayosaidia kuhifadhi miundombinu ya barabara na madaraja.

Kutokana na hayo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa  Remidius Emmanuel amesema Wilaya  yake inaendelea kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kutunza mazingira kwa kuhimiza kutokata miti, kutoharibu vyanzo vya maji, kutovamia misitu.

Amesema kwa kutilia mkazo jambo hilo tayari Wilaya hiyo  imepanda miti na kuhifadhi visiki asili 1,470,252 ambavyo vimeainishwa na kutunzwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments