WALIOSABABISHA MADHARA YA CHANJO KWA MIFUGO WASAKWA

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akikagua eneo lenye kidonda mara baada ya ng’ombe kuchonjwa chanjo ya Homa ya Mapafu (CBPP) kwenye mguu na kuelezea masikitiko yake kuwa zoezi hilo halikuendeshwa kitaalamu katika kijiji cha Mlazo kilichopo Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Baadhi ya mizoga ya kondoo waliokufa baada ya kuchomwa chanjo katika Kijiji cha Mlazo kilichopo Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, hali iliyomlazimu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki kuelekeza kutafutwa mara moja kwa wataalamu waliofanya zoezi hilo pamoja na Kampuni ya Agripest Limited iliyoingia mkataba na halmashauri ya wilaya hiyo ili kufikishwa katika Baraza la Veterinari Tanzania kwa uchunguzi zaidi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Vidonda na uvimbe unavyoonekana kwa baadhi ya ng’ombe waliochomwa chanjo ya Homa ya Mapafu (CBPP) katika Kijiji cha Mlazo kilichopo Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Vidonda na uvimbe unavyoonekana kwa baadhi ya ng’ombe waliochomwa chanjo ya Homa ya Mapafu (CBPP) katika Kijiji cha Mlazo kilichopo Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (aliyeshika fimbo) akizungumza na baadhi ya wafugaji katika Kijiji cha Mlazo kilichopo Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma na kubainisha umuhimu wa chanjo za mifugo dhidi ya magonjwa mbalimbali lakini pia akitaka chanjo hizo kutolewa kitaalamu kwa kufuata mwongozo wa chanjo uliotolewa na wizara juu ya taratibu na kanuni za chanjo. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, akiangalia stakabadhi walizopatiwa baadhi ya wafugaji wa kijiji cha Mlazo kilichopo Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, baada ya kutozwa faini kwa madai ya kutopeleka mifugo kupewa chanjo, huku baadhi yao wakidai hawakupatiwa stakabadhi. Waziri Ndaki amewafahamisha kuwa stakabadhi hizo hazitambuliki na serikali kwa kuwa kwa sasa serikali inatumia stakabadhi za kieletroniki na kuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kufanya uchunguzi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga akizungumza na baadhi ya wafugaji (hawapo pichani) katika kijiji cha Mlazo kilichopo Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma na kusikitishwa na wataalamu waliotoa chanjo ya Homa ya Mapafu (CBPP) kwa mifugo katika kijiji hicho kwa kutofuata taratibu za chanjo hiyo na kutumia sindano ndefu na kuchoma maeneo ya kwenye miguu badala ya shingoni kwenye ngozi nene kwa kutumia sindano fupi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).Na. Edward Kondela

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameagiza kutafutwa mara moja kwa wataalamu wa mifugo waliotoa chanjo ya mifugo katika Kijiji cha Mlazo Kilichopo Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, na kusababisha baadhi ya mifugo kufa na mingine kupata madhara, kufikishwa kwa Baraza la Veterinari Tanzania kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

 

Waziri Ndaki amebainisha hayo (31.08.2021) alipofika katika Kijiji hicho mara baada ya kupatiwa taarifa juu ya madhara yaliyojitokeza baada ya mifugo hiyo kupatiwa chanjo ya Homa ya Mapafu (CBPP) na kusababisha vifo 25 vya ng’ombe, 33 walitoa mimba na waliovimba sehemu waliyochomwa sindano 58, kwa upande wa mbuzi alikufa mmoja, waliovimba watano, waliotoa mimba 12 na upande wa kondoo waliokufa 20, waliovimba 16 na waliotoa mimba watano.

 

Kufuatia hali hiyo na kushuhudia baadhi ya ng’ombe waliopata madhara, Waziri Ndaki amesema zoezi la chanjo ya mifugo dhidi ya magonjwa linaloendelea nchini lina lengo zuri, lakini amesikitishwa na zoezi lililofanywa katika Kijiji hicho cha Mlazo kwa kuwa halikufanywa kwa kuzingatia kanuni za kitaalamu na kuagiza pia Kampuni ya Agristeps Limited iliyoingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwa ajili ya kusimamia zoezi la utoaji chanjo, kuzuiwa kuendelea kutoa chanjo katika wilaya hiyo na kufikishwa kwa Baraza la Veterinari Tanzania kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

 

“Wale wataalamu waliochanja ng’ombe wa hawa wafugaji, watafutwe majina yao, wamesomea wapi, wapelekwe kwa Msajili wa Baraza la Veterinari Tanzania hatuwezi kuendelea kuua ng’ombe namna hii, hii kampuni ilitakiwa ijiridhishe na utaratibu na mchakato mzima wa uchomaji wa chanjo kwa kuwa amefanya kazi hii hapa kuwa mbovu asimame kuendelea kutoa chanjo kwenye Wilaya ya Chamwino tafuteni mwingine.” Mhe. Ndaki akiuarifu uongozi wa wilaya.

 

Aidha, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha watoa huduma walioingia nao mikataba ya utoaji chanjo za mifugo dhidi ya magonjwa 13 ya kimkakati, yanafuata taratibu za utoaji wa chanjo zinaoendelea kutolewa kote nchini kwa kuwa wizara ilishatoa mwongozo wa utoaji chanjo.

 

Kuhusu mifugo inayopata madhara na mingine kufa wakati wa utoaji chanjo kutokana na sababu mbalimbali Waziri Ndaki amesema kuna haja ya kubadilisha Sheria ya Veterinari ya Mwaka 2003 na Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya Mwaka 2003 ili endapo mifugo ikipata madhara yoyote mfugaji aweze kufidiwa mifugo hiyo.

 

Pia, ameutaka uongozi wa Wilaya ya Chamwino kutoendelea kutoa chanjo katika Kijiji cha Mlazo hadi wataalamu watakapotoa elimu ya kutosha kwa wafugaji hao kwa kuwa kwa sasa wamekosa imani kutokana na watu wachache walioendesha vibaya zoezi hilo lililosababisha madhara kwa mifugo kufa na mingine kupata madhara mbalimbali.

 

Akizungumza na wafugaji katika Kijiji cha Mlazo, Waziri Ndaki amesikitishwa pia na malalamiko kutoka kwa wafugaji hao kuwa zoezi hilo la utoaji chanjo kwa mifugo lilienda sambamba na ulipaji wa faini kwa mifugo ambayo inaelezwa haikupelekwa kupata chanjo na kutolewa stakabadhi ambazo siyo za kieletroniki na wengine kulipa faini bila kupatiwa stakabadhi.

 

Kutokana na suala hilo amewaonya watu wanaotumia kigezo cha wafugaji kuwa chanzo cha mapato yao binafsi kwa kuwalipisha faini zisizo halali na kuelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Wilaya ya Chamwino kusimamia suala hilo kabla hajalipeleka katika ngazi ya juu zaidi.

 

“Hili suala la nyinyi wafugaji tunalipeleka TAKUKURU na kama hakuna kinachotokea tutatafuta TAKUKURU iliyo juu ya TAKUKURU hatuwezi kuwa na TAKUKURU ya Chamwino inakuja kuchunguza inaondoka moja kwa moja na ushahidi uko hapa serikali kwa sasa inatumia risiti za kieletroniki siyo za kuandika kwa mkono na pesa zote hizi wanatozwa wafugaji.” Amebainisha Waziri Ndaki

 

Akizungumzia juu ya utaratibu wa utoaji wa chanjo ya mifugo dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu (CBPP) iliyoleta madhara kwa baadhi ya mifugo ya wafugaji wa Kijiji cha Mlazo, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amesema, uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa sindano zilizotumika zilikuwa ndefu na kwamba mifugo ilipaswa kuchomwa chini ya ngozi maeneo ya shingoni ambapo kuna ngozi nene na siyo kwenye mguu ambapo ngozi yake ni nyembamba kwa kuwa chanjo hiyo haipaswi kugusa nyama.

 

Prof. Nonga amefafanua kuwa chanjo hiyo imeelekeza kuwa endapo ikiingia ndani ya nyama inasababisha nyama kuharibika kwa kuwa inaua seli za mwili kama ambavyo imefanyika kwa baadhi ya mifugo kupata uvimbe, majipu na usaha maeneo ambayo imechomwa chanjo.

 

Baadhi ya wafugaji waliopata fursa ya kuzungumza katika kikao hicho na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki wamesema zoezi la chanjo lililofanywa katika Kijiji chao cha Mlazo Tarehe 19 Mwezi Julai Mwaka 2021 halikuwa shirikishwaji kwa kuwa hapakutolewa elimu yoyote juu ya chanjo hiyo na kwamba walikuwa wakitozwa faini na kutishiwa na viongozi wa kijiji.

 

Pia wamelalamikia kitendo cha kutokuwepo kwa ushirikiano kati ya viongozi wa kijiji na wananchi kwa kuwa walikuwa wakichangisha fedha kwa ajili ya chanjo na hata baada ya mifugo yao kupata madhara hakuna msaada wowote ambao wamepata kutoka kwa viongozi wao, ambao hawakushiriki pia katika kikao cha Waziri Ndaki na hata walipotafutwa hawakujulikana walipo.

 

Pia wamesikitishwa licha ya kutopata msaada juu ya madhara waliyopata kwa mifugo yao, bado walikuwa wamearifiwa kuwa chanjo hiyo itatolewa tena Tarehe 15 Mwezi Septemba mwaka huu, huku wakihofia kuendelea kupoteza mifugo kwa kufa na mingine kupata madhara mbalimbali, ambapo tayari Waziri Ndaki ametoa maelekezo ya kutofanyika chanjo yoyote katika kijiji hicho hadi elimu zaidi itolewe na kuagiza wataalamu waliotoa chanjo awali kutafutwa pamoja na Kampuni ya Agristeps Limited iliyoingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na kufikishwa kwa Baraza la Veterinari Tanzania kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

 Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post