DKT. MREMA AYATAKA MADHEHEBU YA DINI KUELIMISHA WAUMINI CHANJO YA COVID-19 - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Sunday, September 5, 2021

DKT. MREMA AYATAKA MADHEHEBU YA DINI KUELIMISHA WAUMINI CHANJO YA COVID-19

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mstaafu, Dkt. Augustino Mrema, akizungumza jana wakati wa misa takatifu ya shukrani kwa ajili kubariki nyumba yake na za watoto wake alizozijenga eneo la Salasala jijini Dar es Salaam.
Misa hiyo takatifu ya shukrani ikiendelea.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi mstaafu, Dkt. Augustino Mrema akiwa na familia yake wakati wa misa hiyo. 


Na Dotto Mwaibale


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi mstaafu, Dkt. Augustino Mrema, ameyataka madhehebu na viongozi wa dini nchini kuendelea kuwaelimisha waumini wao umuhimu wa kupata chanjo ya COVID-19 na kuchukua tahadhari za ugonjwa huo kama ambavyo wataalam wa afya wanashauri.

Akizungumza jana wakati wa misa takatifu ya shukrani kwa ajili kubariki nyumba yake na za watoto wake alizozijenga eneo la Salasala jijini Dar es Salaam, alisema janga la Corona lipo hivyo kila mtu ahakikishe anachukua tahadhari.

"Napenda kulishukru Kanisa Katoriki kwa kutoa elimu kwa waumini wao juu ya umuhimu wa chanjo ya Corona ambayo ni hiari kwa anayetaka na shukrani za kipekee zimwendee Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu  Yuda Ruwai'chi ambaye amewahimiza mapdri kupata chanjo," alisema.

Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), alisema watanzania waepuke propaganda zinazotolewa na baadhi ya watu wanaopinga chanjo ya Corona wakati serikali imeileta ili kutusaidia kukabiliana na ugonjwa huo.

"Ruwai'chi yeye sio kiongozi wa siasa lakini anahimiza mapdri na waumini kuchanja chanjo ya corona, chanjo ni muhimu sana na ukinga watu wote wenye ugonjwa kisukari, presha, kifua Kikuu pamoja na watu wenye umri wa miaka 60 kuchangamkia chanjo mapema kwani zinatolewa bure bila malipo" alisema.

Mrema alisema siyo mara ya kwanza kwa wananchi wa Tanzania kupata chanjo lakini inashangaza chanjo hii ya UVIKO-19 imekuwa na upinzani mkali sana na cha kushangaza miongoni mwa wanaopinga ni viongozi wa kisiasa.

" Kuchanja sawa na polisi anapokwambia funga mkanda unapokuwa kwenye gari, anakusaidia ili hata ukipata ajali huwezi kuumia sana sababu mkanda utakuzuia, " alisema.

Mrema alisema hofu ya kwamba waliochanjwa baada ya muda watakuwa mazombi hizo ni kauli kuwatia hofu kwani wataalamu waliobobea na masuala ya afya duniani wameshathibitisha kuwa chanjo hiyo ni salama.

Alisema hakuna sababu ya kuingiwa na hofu katika suala hili kwani bahati nzuri hata rais Samia Suluhu Hassan ameonesha njia kwa kupata chanjo hiyo ambayo inaendelea kutolewa katika nchi kadhaa duniani.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti zaidi ya watu 300,000 wameshapata chanzo nchini.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages