IMF YAIPATIA TANZANIA DOLA MILIONI 567.3 KWA AJILI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA UVIKO 19

 

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUIDHINISHWA KWA FEDHA ZA MKOPO NAFUU WA KUKABILIANA NA ATHARI ZA UVIKO-19 KUTOKA IMF

DODOMA: Tarehe 8 Septemba, 2021:  BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeridhia kutoa mkopo nafuu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa jumla ya dola za Marekani milioni 567.25 sawa na shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya kukabliana na athari za UVIKO-19.

Fedha hizo zinajumuisha mkopo nafuu usio na riba kupitia dirisha la Rapid Credit Facility (RCF) wa jumla ya dola za Marekani milioni 189.08; na mkopo nafuu wenye riba ndogo kupitia dirisha la Rapid Financing Instrument (RFI) wa dola za Marekani milioni 378.17.

Fedha hizo zitatumika ndani ya mwaka huu wa fedha katika kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zitokanazo na UVIKO-19.

Sekta zitakazonufaika kulingana na makubaliano yetu na IMF ni afya, elimu, utalii, maji, pamoja na kusaidia kaya maskini kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii (TASAF) na kuwezesha makundi maalum ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Kila sekta itatumia fedha hizo kwenye masuala yanayolenga kukabiliana na na athari za UVIKO-19 ambapo pamoja na mambo mengine, Sekta ya afya itanunua dawa na vifaa tiba vya kupambana na UVIKO-19 na kugharamia utekelezaji wa mpango wa chanjo.

Sekta ya elimu itaweka mazingira yatakayowezesha wanafunzi kujifunza bila msongamano na kuchukua tahadhari ya maambukizi ya UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maboma ya shule na kuongeza madawati.

Sekta ya maji itaongeza miundombinu ya maji itakayowezesha upatikanaji wa huduma ya maji tiririka kwa wingi zaidi mijini na vijijini; na Mpango unaoendelea wa TASAF utaongezewa fedha (Complement) ili kusaidia kaya maskini zilizoathirika na UVIKO 19.

Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) itawezeshwa pia kukabiliana na athari za UVIKO-19 katika sekta zilizoathirika ikiwa ni pamoja na afya, utalii na kilimo.

Waziri mwenye dhamana ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameziasa sekta zote zitakazopata fedha hizi kuzitumia kulingana na Mpango tulioandaa kwa pamoja na sekta husika wa kukabiliana na athari za UVIKO-19 – Tanzania COVID-19 Socio-Economic Recovery and Response Plan (TCRP). Aidha, fedha hizo zitumike kwa kuzingatia makubaliano yetu na IMF kama ilivyoainishwa kwenye barua ya dhamira ya Serikali (Letter of Intent - LOI) ikiwa ni pamoja na utoaji wa taarifa za utekelezaji kwa wakati.

 

Imetolewa na:

Benny Mwaipaja

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments