CHARAHANI ATOBOA KURA ZA MAONI UBUNGE CCM JIMBO LA USHETU, AWABWAGA WENZAKE 18

Emmanuel Charahani

Na Salvatory Ntandu - Kahama
Emmanuel Charahani ameibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha kura za maoni katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano mkuu wa jimbo la Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga kwa kupata kura 442 na kuwashinda wenzake 18.

Akitangaza matokeo ya kura za maoni za jimbo hilo, msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, James Kusekwa amesema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki ambapo wagombea wote waliridhika na kusaini matokeo ya jimbo hilo lenye wajumbe 880.

Kusekwa aliwataja watia nia wengine walioshiriki uchaguzi huo kuwa ni pamoja na Makoye Mayenga aliyepata kura 143,Alhad Mlyansi kura 125,J ames Lembeli kura 56, Dk. Lamek Makoye kura 16 na Samson Lutonja kura 11.

Wengine ni pamoja na Ernest Nila kura 8 ,Bundala Shija kura 11 Dk Mathew Masele kura tano, Merry Lema kura tano Bether Juma kura tatu,Ahmed Haroun kura tatu,Michael Paschal kura mbili, Balindo Jordani kura moja, na Martine Mwakatundu kura 0.

Wakizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo baadhi ya watia nia wa jimbo hilo akiwemo Betha Juma amewataka wagombea wenzake kuvunja makundi yaliyokuwepo wakati wa kura za maoni na badala yake wamuunge mkono mgombea yeyote atakayeteuliwa na tume.

“Tuvunje makundi kuanzia leo,sisi ni wamoja na wajumbe wametupanga kwa uwezo wetu, jina lolote litakalorudishwa na chama sisi tutakuwa mstari wa mbele kumtafutia kura ili chama chetu kiweze kushinda katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Oktoba tisa mwaka huu”, amesema Juma.

Dk Yohana Masonda amesema wataendelea kuheshimu maamuzi ya wajumbe wa mkutano huo mkuu wa jimbo kwa kumchagua Charahani kuongoza katika kura za maoni na kuwataka wagombea wenzake kuwa na ummoja na mshikamano na kuachana na makundi yasiyokuwa na tija.

Awali akiwashukuru wajumbe wa mkutano huo, Emmanuel Charahani amesema kuwa atahakikisha anashirikiana na wagombea wengine katika kutafuta kura za CCM kwa atakayepitishwa na chama kupeperusha bendera katika uchaguzi mdogo ujao.

“Niwahakikishie mimi nitaendelea kushirikiana nanyi katika kutafuta maendeleo ya wakazi wa jimbo la Ushetu,bado tunachangomoto nyingi tunapaswa kuzitatua ili wananchi wetu waweze kupata maendeleo hususani katika sekta za afya,maji,umeme na miundombinu ya barabara,”amesema Charahani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post