MTANDAO WA JINSIA TANZANIA 'TGNP' WAMPONGEZA RAIS SAMIA KWA TEUZI ZENYE KUZINGATIA JINSIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. Stergomena Tax kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 13 Septemba, 2021.

PONGEZI KWA MH. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, SAMIA SULUHU HASSANI KWA TEUZI ZENYE KUZINGATIA JINSIA. 


Kwa niaba ya wanachama, bodi ya wakurugenzi na wafanyakazi/watumishi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP), kwa furaha kubwa sana tunapenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassani kwa kuendelea kuzingatia jinsia katika uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi uliofanyika tarehe 12 Septemba 2021. Katika uteuzi huo, Mhe. Rais aliteua viongozi watano, mawaziri wanne (wanawake wawili na wanaume wawili) na hivyo, kufikia asilimia 50/50 ya uteuzi huo wa mawaziri. Pia, alimteua Mwanasheria Mkuu wa serikali ambaye ni mwanaume. Kwa ujumla, Mhe. Rais aliteua wanawake wawili sawa na asilimia 40 na wanaume watatu, sawa na asilimia 60.


Mbali na kuzingatia idadi ya wanawake katika uteuzi huu, tunatambua jitihada za Mhe. Rais kuhakikisha pia kuwa wanawake wanashika nafasi muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu, nafasi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikishikiliwa na wanaume. Katika uteuzi huu, kwa mara ya kwanza nchi yetu imetengeeneza kestoria kwa kuwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye ni mwanamke, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrance Tax.


Dkt. Tax anakuwa mwanamke wa tatu kushika nafasi ya Uwaziri Ulinzi Afrika Mashariki, ambapo mawaziri wawili wanawake wanatoka nchini Kenya; Raychelle Omamo (May 2013- Januari 2020) na Monica Juma (Jan 2020 hadi sasa).


  Pia, nchi yetu imetengeneza kestoria kwa kuwa na mwanamke wa kwanza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji. Wizara hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetokana na marekebisho yaliyofanywa na Mh. Rais baada ya kuhamisha idara ya habari kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia. Hatua hii ni kubwa sana katika historia ya harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi nchini na Afrika kwa ujumla. 


Kwa ujumla, uteuzi huu umeongeza nafasi za wanawake mawaziri kufikia 7 sawa na asilimia 30.4 kutoka 5 sawa na asilimia 21.7 wakati huo wanaume wakiwa ni 16 sawa na asilimia 69.6 kutoka 18 sawa na asilimia 78.2 mwezi Marchi 2021 Mhe Rais aliposimikwa rasmi kama Rais wa awamu ya sita na kufanya mabadiliko madogo kwenye baraza la mawaziri lililoundwa na mtangulizi wake Rais John Pombe Magufuli.

Tunatoa wito kwa viongozi wanawake na wanaume walioteuliwa na Mh. Rais kutumia nafasi na taaluma zao vyema kumsaidia Mhe. Rais kutimiza majukumu yake ya kuleta maendeleo endelevu na jumuishi nchini. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments