RC MTAKA, WAKUU WA WILAYA WASAINI MKATABA MASUALA YA LISHE DODOMA...AHIMIZA WANANCHI WACHANGAMKIE KILIMO CHA KISASA


Na Dotto Kwilasa - Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesaini Mkataba baina yake na Wakuu wa Wilaya Saba za Mkoa huu kuhusu makubaliano ya kuwekeza katika masuala ya lishe  huku akiwataka Wakuu hao wa Wilaya kuwahimiza Wakulima Mkoani Dodoma kuchukulia changamoto za masuala ya lishe kuwa fursa kwao na kuona umuhimu wa kuanza kulima bidhaa za chakula lishe.

Hayo yamejiri leo Jijini Dodoma katika  Warsha ya wadau wa lishe Kupitia mradi wa USAID/Lishe endelevu unaotekelezwa katika mikoa ya Rukwa,Iringa,Dodoma na Morogoro.

Wakuu hao wa Wilaya waliotia Saini Mkataba huo ni Mwanahamisi Mkunda(Bahi),Simon Chacha(Chemba),Jabir Shekimweri (Dodoma Jiji),Gift Msuya (Chamwino),Dkt Hamis Mkanachi(Kondoa),Remidius Mwema(Kongwa)na Josephat Maganga(Kongwa).

Mtaka amesema kama Mkoa hali ya lishe bado hairidhishi hivyo kutumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi wa Mkoa wa Dodoma hususani wakulima kutilia mkazo kilimo cha kisasa kitakacholeta tija kwa masuala ya lishe .

"Ni wakati wa kuzingatia Kilimo bora cha kisasa kitakacholeta tija kwa lishe ya watanzania,acheni kilimo cha mazoea,"amesema.

Kwa upande wake Katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma Dkt.Fatma Mganga amewaomba wakuu hao wa Wilaya kutoa ushirikiano kwa kuwasaidia kuboresha hali ya lishe katika maeneo yao ambapo amedai kwa Sasa hali ya lishe sio nzuri.

Amesema,baadhi ya wadau Wakuu wa masuala ya lishe bado hawatilii maanani suala Hilo na kwamba inapotokea wanahitajika katika vikao mara nyingi hawahudhurii na badala yake huishi kuwatuma wawakilishi.

"Tukiwa Kwenye kikao Kahama tuliona wenzetu wanachukua makombe ila tuliwaambia na sisi tutakuja kuchukua katika siku za baadae ,sasa tumeanza safari ya miaka mitano Kwa ajili ya kuboreshà lishe kwa mkoa wa Dodoma
niwaombe tukasimamie viashiria vyote,"amesema.

Naye Meneja  wa Shirika la Save the Children Dodoma Gideon Muganda ameeleza kuwa  ili kuwepo kwa maendeleo yatakayochochea uchumi,lazima kuwepo na juhudi za kuwezesha huduma za lishe kwa wanawake na watoto.

Hatua hii pia itasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali katika Kupunguza tatizo la utapiamlo na udumavu ambalo bado kinawasumbua watoto kwa kiasi kikubwa.

Meneja huyo ameeleza kuwa licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuwekeza katika lishe bado jitihada zaidi zinahitajika ikiwa ni pamoja na kuungalia upya mpango mkakati unaohusisha mfumo wa muundo wa lishe .

Mbali na hayo ameeleza malengo matatu ya warsha hiyo kuwa ni pamoja na kuimarisha Sekta mtambuka ya lishe ili kuimarisha Afya,Usafi,matumizi ya Maji safi na salama kwa watoto ,uzalishaji wa chakula chenye tija pamoja na kurahisisha upatikanaji wa chakula kitakachowezesha Jamii kula mlo kamili na vyakula vya asili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments