WANAHABARI WAELEZENI UKWELI WANANCHI JUU YA CHANJO YA UVIKO 19

 Na Fabian Fanuel - Mtandaoni

 Wahabari nchini wametakiwa kuwatumia wataalamu wa afya katika kutoa habari zinazohusiana na UVIKO 19 na kuacha kuwapa nafasi watu wasio na taaluma ya afya kuuzungumzia ugonjwa huo ili kuondoa sintofahamu inayoendelea nchini juu ya chanjo ya Covid 19.


Kauli hiyo imetolewa leo na madaktari bingwa wa Muhimbili na Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete wakati wa mkutano wa Zoom ulioandaliwa na Klabu  ya  Waandishi wa  Habari ya  Mkoa wa Mwanza  kwa kushirikiana na  Taasisi ya Freedom  House.


Akifungua kikao hicho Mkurugenzi wa tiba kutoka Wizara ya Afya Dr leornard Subi kwa niaba ya Waziri Afya Jinsia Wazee na Watoto Dr Dorothy Gwajima, amesema hadi sasa kuna matokeo mazuri ya chanjo ya UVIKO 19 tangu ilipoanza kutolewa hapa nchini ambapo hadi sasa kuna vituo zaidi ya 1845 vinavyotoa huduma ya chanjo kote nchini na jitihada za kufika mpaka vijijini zinaendelea.


Dr Subi amesema Tanzania imepunguza idadi ya vifo tangu Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,Rais Samia Suluhu Hassan alipozindua uchanjaji wa chanjo July 28 mwaka huu na kuwataka watanzania kuendelea kujitokeza katika vituo vilivyotengwa kwaajili ya kupata chanjo ili kupunguza makali ya ugonjwa huo wa UVIKO 19.


Akizungumzia umuhimu wa chanjo ya Covid 19 Profesa Harun Nyagori ambae ni Daktari bingwa mwandamizi wa magonjwa ya ndani na moyo kutoka (JKCI) amesema chanjo ya UVIKO 19 ni salama na haina madhara  yoyote kwenye mifumo ya uzazi wala haisababishi kuganda kwa damu kama inavyoelezwa.


Profesa Nyagori amesema tafiti zote zilizofanywa hazionyeshi mtu atakayepatiwa chanjo ya UVIKO 19 atapata tatizo la uzazi na badala yake ilionekana kuna wanaume walipungukiwa nguvu za kiume baada kukutwa virus vya UVIKO 19 ambapo waliathirika asilimia 18 tu na baada ya kupatiwa chanjo watu hawa hurudi katika hali zao za kawaida.


Akizungumzia kuhusiana na fununu za kuganda kwa damu Profesa Nyagori amesema kitaalamu ugonjwa wenyewe wa UVIKO 19 unaweza kusababisha kuganda kwa damu kwa mgonjwa kwa asilimia 15 lakini pia akasema kuna magonjwa mengine ambayo ni kisukari na presha husababisha damu kuganda hivyo sio sahihi kudhani kwamba chanjo inaweza kusababisha tatizo hilo.


Naye mkurugenzi wa shirika la Freedom House Daniel Lema ameishukuru wizara ya afya kwa kutoa wataalamu ambao wameweza kutoa wataalamu ambao wametoa majibu ya maswali ambayo yamekuwa yakiulizwa na jamii juu ya chanjo ya UVIKO 19.


Lema amewataka wataalamu kuendelewa kutoa elimu kwa jamii ili kutoruhusu uvumi wa taarifa zisizo na ukweli kupata nguvu kutoka kwa watu ambao wanalengo baya la kupotosha ukweli uliopo.


Naye Mwenyekiti wa  MPC bwana  Edwin Soko amewashuru wadau  wote  kwa  kuhudhuria  mkutano huo na kusema kuwa, watajitahidi  kukaanda  mikutano  kama  hiyo  ili  kujadili  mwenendo  wa  chanjo  ya  UVIKO 19 na  umuhimu wa kuchanja.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments