ASKARI MAGEREZA AKAMATWA AKIJIUA BAADA YA KUBAKA NA KULAWITI KWA ZAMU NA MWENZAKE

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala ACP Debora Magiligimba

Na Mwandishi wa Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala linamshikilia Askari wa Jeshi la Magereza mwenye namba B 9780 WDR Said Hassan Said (26) , Mkazi wa Ukonga kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka 29 (jina linahifadhiwa).

Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala ACP Debora Magiligimba tukio hilo limetokea Septemba 1,2021 majira ya saa tano nusu usiku katika barabara ya madafu Ukonga jijini Dar es salaam.

"Mtuhumiwa huyo ambaye ni askari wa Jeshi la Magereza mwenye namba B 9780 WDR Said Hassan akiwa na mwenzake ambaye bado hajakamatwa walimkamata kwa nguvu binti huyo na kumuingiza kwenye gari dogo kisha kuondoka naye hadi kwenye nyumba moja iliyopo karibu na kambi ya KMKM Ukonga Magereza na kuanza kumbaka na kumlawiti kwa zamu", ameeleza Kamanda Magiligimba.

"Baada ya kumaliza kumbaka na kumlawiti watuhumiwa hao waliendelea kumfanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kumwingizia mkono katika sehemu zake za siri na kumsababishia majeraha makubwa na maumivu makali katika sehehmu zake za siri",ameongeza Kamanda Magiligimba.

Amefafanua kuwa baada ya mtuhumiwa kugundua kuwa anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa tukio baya alilolifanya na mwenzake, mnamo tarehe 02/09/2021 alijaribu kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila na kuacha ujumbe wa maandishi kwa mkuu wake wa kazi na askari wenzake kuwa “mnisamehe bure kwa uamuzi wangu niliochukua kwa tukio nililolifanya nitaonekana nimekufa kizembe” ujumbe ambao ulikuwa unamlenga mkuu wake wa kazi na wafanya kazi wenzake.

Hata hivyo kabla mtuhumiwa huyo hajafanikisha azma yake ya kujitoa uhai alikamatwa na kufikishwa kituo cha Polisi.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala linaendelea na msako mkali kwa mtuhumiwa mwenzake aliyekimbia baada ya tukio hilo baya na linamtaka ajisalimishe haraka iwezekanavyo katika kituo chochote cha Polisi", amesema Kamanda Magiligimba.

Ametoa wito kwa wananchi kuacha kuwatendea vitendo vya ukatili na udhalilishaji wanawake na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa juu ya matukio ya ukatili wa kijinsia ambayo yana waathiri kimwili na kisaikolojia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments