MFANYAKAZI WA BENKI YA CRDB ANUSURIKA KUFA KWA KUPIGWA, KUKATWA MKONO....ABEBWA AMEZIMIA SHINYANGA HADI KAHAMA - MALUNDE 1 BLOG | Fahari ya Shinyanga

Breaking

Saturday, September 11, 2021

MFANYAKAZI WA BENKI YA CRDB ANUSURIKA KUFA KWA KUPIGWA, KUKATWA MKONO....ABEBWA AMEZIMIA SHINYANGA HADI KAHAMA

Picha haihusiani na habari hapa chini

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mfanyakazi wa Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi Debora Rwekwama (34) mkazi wa Bushushu Mjini Shinyanga amefanyiwa ukatili kwa kushambuliwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kukatwa mkono wa kushoto kwa kisu na mme wake aitwaye Jacobo Mwajenga (35) kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema tukio hilo limetokea Septemba 9,2021 usiku katika mtaa wa Bushushu, Manispaa ya Shinyanga.

“Usiku wa Septemba 9,2021 Mfanyakazi wa Benki ya CRDB Debora Rwekwama (34) (Banker - CRDB)  mkazi wa Bushushu Manispaa ya Shinyanga alishambuliwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na baada ya kupoteza fahamu alikatwa mkono wa kushoto kwa kisu na mme wake aitwaye Jacobo Mwajenga (35)mkazi wa Bushushu”,amesema Kamanda Kyando.

"Huyu Jacob Mwajega inasemekana siku ya tukio mchana alienda pale Benki ya CRDB Mjini Shinyanga akakuta mke wake hayupo pale Benki isipokuwa Hand bag (Mkoba)  wake upo, huyu bwana akamsubiri mkewe, akiwa pale ukataka kutokea mzozo kidogo pale lakini watu wakaingilia kati kwamba haya mambo hayafai sehemu za kazi mtaenda kuyaongea huko nyumbani kwenu",ameeleza 

"Kwa hiyo usiku huo huyu bwana Jacobo Mwajenga akamshambulia huyo mke wake  na kusababisha azimie na kumkata jeraha kubwa kweli kweli kwenye mkono wake wa kushoto na kusababisha mama huyu kuvuja damu nyingi",ameongeza

Baada ya kufanya tukio hilo, Bushushu Mjini Shinyanga Jacobo Mwajenga akambeba mke wake akiwa amezimia na kumpakia kwenye gari yao na kumpeleka hadi katika kituo cha Polisi Kahama.

"Alipofika katika kituo cha polisi Kahama akaripoti kwamba huyu mama amepata ajali, kutokana na hali aliyokuwa nayo mama huyo polisi hawakumhoji kwani alikuwa amezimia walichokifanya ni kumpa PF3 ili huyo bwana amkimbize mwanamke huyo hospitali na hawakujua kama ni mme wake",amesema.

"Huyu bwana akampeleka mama huyu hospitali ya wilaya ya Kahama. Sasa madaktari walivyokuwa wanamchunguza mama huyu hawakuona dalili ya ajali wakabaini kuwa mama ameshambuliwa wakatoa taarifa polisi na Polisi tukamkamata huyu bwana Jacobo akiwa hapo hospitali",amesema Kamanda Kyando.

Amesema chanzo cha tukio ni wivu wa mapenzi na kwamba tayari Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa wa tukio hilo.

"Chanzo cha tukio hili ni wivu wa mapenzi. Huyu bwana yeye ni anafanya kazi ya Kuongoza watalii kule Arusha. Na kutokana na hii changamoto ya ugonjwa wa Corona inaonekana kazi yake imepata shida, muda mrefu yupo hapa Shinyanga anaishi na mke wake, hajishughulishi na kazi yoyote. Mama ni mfanyakazi wa Benki yeye yupo tu nyumbani,kwa hiyo nafikiri akajenga tabia ya wivu, na tumebaini chanzo cha tukio hili ni wivu wa mapenzi", ameeleza Kamanda Kyando.

Ameeleza kuwa hali ya majeruhi ni mbaya na amelazwa katika hospitali ya wilaya Kahama.

Kamanda Kyando amesema hivi sasa kuna matukio mengi ya vifo vinavyotokana na wivu wa mapenzi hivyo kutoa wito kwamba ukigundua kuwa mwenzako siyo mwaminifu kwenye mapenzi usijichukulie sheria mkononi,nenda kwa viongozi wa dini,serikali au vyombo vya dola kuliko kuchukua sheria mkononi kwani ni kosa la jinai na matokeo yake kuishia jela.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553

No comments:

Post a Comment

Pages