FISI AUA MTOTO WA MIAKA MITATU SHINYANGA MJINI


Mtoto aliyejulikana kwa jina la Raphael Juma Dotto mwenye umri wa miaka mitatu amefariki dunia baada ya kushambuliwa na mnyama Fisi wakati akicheza nyumba ya jirani na watoto wenzake katika mtaa wa Majengo Mapya kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa mtaa wa Majengo mapya, Mohammed Mlabu amesema tukio hilo limetokea jana Jumamosi Septemba 25,2021 majira ya saa moja usiku.

"Majira ya saa moja usiku alitokea fisi na kukuta watoto wanacheza nje ya nyumba jirani, wazazi hawakuwepo, fisi huyo alimchukua mtoto wa miaka mitatu na kukimbia naye, watu walipomfuatilia,fisi akakimbia wakakuta amejeruhiwa kwa kuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

"Wazazi hawakuwepo, watoto ndiyo walitoa taarifa kuwa flani kachukuliwa na fisi, bodaboda wakasaidia kumfuatilia huyo fisi na tukashirikiana nao kumpeleka mtoto huyu hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu bahati mbaya mtoto akafariki dunia majira ya saa sita usiku", ameeleza Mlabu akizungumza na Malunde 1 blog.

"Kumekuwa na fisi wengi sana kwenye eneo hili , fisi wanazunguka kuanzia saa moja usiku na tumekuwa tukiwaambia watu wa Mali asili waje tufanye msako wa fisi lakini ushirikiano umekuwa hafifu kwani wao wamekuwa wakituambia kuwa tukiona fisi ndiyo tuwape taarifa waje", ameongeza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments