GGML YATOA MAFUNZO YA COVID-19 KWA WAANDISHI WA HABARI 60


Makamu Rais wa GGML, Simon Shayo akifungua mafunzo hayo
Jimmy Mtabwa ambaye ni mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita akizungumza katika mafunzo hayo ya waandishi wa habari mkoa wa Geita.
Katibu Mtendaji wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita, Novatus Lyaruu akizungumza katika mafunzo hayo.
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mafunzo hayo

Na mwandishi wetu
Kampuni ya uchimbaji wa Madini ya Dhahabu mkoani Geita (GGML) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari 60 wa Geita ili kuwajengea uelewa kuhusu maambukizi ya virusi vya Corona.

Mafunzo hayo yaliyotolewa jana Mjini Geita, pia yamelenga kuwakumbusha waandishi wa habari umuhimu wa chanjo ya Corona.

Akifungua mafunzo hayo, Makamu wa Rais wa GGML anayesimamia miradi endelevu ya kampuni, Simon Shayo amesema GGML mbali na kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuchangia fedha za kudhibiti ugonjwa huo, imeona ni vema kufadhili mafunzo hayo ili kuwajengea uelewa wa kutosha waandishi wa habari.

Alisema moja ya jukumu la kampuni ni kuhakikisha jamii zinazoizunguka zinanufaika kutokana na uwepo wa GGML mahala hapa.

“Kwa hivyo, tumeamua kutumia mikakati tofauti kuendesha kampeni za uhamasishaji namna ya kujikinga na janga la UVIKO-19 na tumeungana na mikakati mbalimbali ya Serikali kuhamasisha watu wengi kuzingatia hatua, vigezo na taratibu zinazotolewa na watalaam wa afya wa Serikali ikiwamo umuhimu wa kupata chanjo.

“Nasema hivi kwa sababu chanjo hizi zina ufanisi mkubwa, na ni muhimu zaidi kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba. Kwa kujilinda sisi wenyewe, tunapunguza athari kubwa ya UVIKO-19 kwa wale wanaotuzunguka. Tumeshuhudia mfano bora ukionyeshwa na viongozi wetu wakuu Kitaifa na hata Kimkoa na Kiwilaya kwa kuchanja hadharani ili kuwapa moyo wananchi wengine wachukue hatua ya kuchanja,” alisema.


Aidha, alisema kama sehemu ya ushirki wake kuunga mkono juhudi za Serikali, GGML ilitoa jumla ya Sh bilioni 1.6 kusaidia juhudi za kupunguza kasi ya kuenea kwa UVIKO-19. Lakini pia masharti na taratibu zilizokuwa zinafuatwa na GGML, zilizingatia miongozo iliyotolewa na Serikali ya Tanzania.

“Kati ya fedha zote zilizotolewa, GGML ilitoa takriban Sh bilioni 1.1 kuchangia mfuko wa kitaifa wa dharura katika kupambana na UVIKO-19. Mfuko huu ulioanzishwa na Serikali ulikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Jumla ya Shilingi milioni 500 zilizobaki zilitumika kusaidia mahitaji mbalimbali ya mkoa na jamii inayotuzunguka hapa Geita hii ikiwa ni pamoja na utoaji wa vifaa tiba na dawa muhimu vikiwemo vya kujikinga kwa watabibu, mitungi ya gesi na kadhalika,” alisema.

Aidha, Jimmy Mtabwa aliyewakilisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wa Geita alitoa wito kwa waandishi wa habari kuungana na serikali katika kuelimisha wananchi kuhusu ugonjwa huo.

Katibu Mtendaji wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani, Geita, Novatus Lyaruu mbali na kuishukuru GGML kwa mafunzo hayo, alisema mafunzo hayo yatawasaidia kupata majawabu ya maswali mengine yaliyokuwa yameibuka kuhusu chanjo ya Johnson &Johnson.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments