RAIS SAMIA : SERIKALI ITAENDESHWA KWA MATENDO MAKALI SIYO MANENO MAKALI 'MSITEGEMEE NIANZE KUFOKA OVYO OVYO'


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi kwenda kwa wananchi kutoa huduma inayotakiwa na kila mtu kufanya wajibu wake
badala ya kutoa maneno makali akisema Serikali itaendeshwa kwa matendo makali siyo maneno makali.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Septemba 13,2021 wakati akiwaapisha Mawaziri Wanne na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Viongozi walioapishwa ni Mhe. Dkt. Stergomena Lawarance Tax (Mb) kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb), kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. January Yusuph Makamba (Mb), kuwa Waziri wa Nishati, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (Mb), kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

"Kipindi cha miezi sita ya uongozi wangu nilikuwa najifunza, Nilikuwa Makamu wa Rais, nilikuwa na nyinyi lakini sikuwa na fursa ya ndani ya kujifunza utendaji wa ndani ya Wizara mbalimbali. Nimekuwa nikijifunza na nimeona sasa vipi nakwenda na nyie. Katika kipindi hiki cha miezi sita ya uongozi wangu, kuna watu walichukulia serikali poa, serikali cool, kwa hiyo wakafanya yale wanayotaka",amesema Rais Samia.

"Katika uongozi kuna mbinu nyingi. Nami nimejichagulia mbinu yangu. Nataka niwaambie kuwa tunakoendelea huko Serikali yetu itaendeshwa kwa matendo makali na siyo maneno makali. Ninaposema matendo makali wala siyo kupigana mikwaju au mijeledi, ni kwenda kwa wananchi kutoa huduma inayotakiwa, kila mtu kufanya wajibu wake",amesema Rais Samia.

"Msinitegemee kwa maumbile yangu haya, pengine na malezi yangu kukaa hapa nianze kufoka weyee..ee..wawawaaaaa! Nahisi siyo heshima, na kwa sababu nafanya kazi na watu wazima, wanaojua jema na baya ni lipi. Kwa hiyo ni imani yangu kwamba tunapozungumza tunaelewana na kila mtu anajua afanye nini kwenye wajibu wake. Kwa hiyo msitegemee nianze kufoka ovyo ovyo, kufokea watu wazima wenzangu, nitafoka kwa kalamu",ameongeza Rais Samia.

Soma pia

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments